Kamati Kuu CCM yacharuka

Yataka wabadhilifu kuchukuliwa hatua

KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeiagiza serikali  kuwachukulia hatua waliohusika kwenye ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan  imetoa maelekezo hayo leo April Mosi, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam ilipokutana kwenye kikao chake cha kawaida.
Ripoti hiyo ya CAG na Takukuru ziliwasilishwa Ikulu, Dar es Salaam, Machi 29, 2023 na kubainisha ubadhirifu wa fedha katika maeneo mbalimbali serikalini.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema akizungumza mara baada ya Kikao hicho cha Kamati amesema kamati kuu imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa upungufu, udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana.
Amesema, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, hali inayosababisha serikali kukosa mapato na kupata hasara, uwepo wa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara na vitendo vya ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, kama vile kuongeza bei za manunuzi ya Serikali.
Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi,” amesema Mjema na kuongeza:
Imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.”
Mjema amesema, kamati kuu ya CCM, imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyetembelea nchi yetu kwa siku tatu kuanzia Machi 29 hadi 31, 2023.
Amesema, ziara hiyo imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya mahusiano yenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button