Kamati viongozi wakuu Zanzibar yazuru Nemc
KAMATI ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia ofisi ya viongozi wakuu wa kitaifa Zanzibar imetembelea ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa masuala ya mazingira.
Kamati hiyo iliyoambatana na timu ya watu 31 imepata fursa ya kutembelea mradi wa treni ya umeme ya SGR kituo kikuu cha Dar es Salaam ili kupata taarifa sahihi za jinsi mradi huo unavyozingatia masuala ya utunzaji wa mazingira.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu Zanzibar, Machano Othman Said amelipongeza baraza hilo kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia mazingira kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na maendeleo kama treni ya umeme SGR.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NEMC, Mhandisi Profesa Esnati Chaggu amesema baraza linazingatia utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira na kanuni zake na kuhakikisha elimu juu ya mazingira inatolewa kwa jamii.
SOMA: Mabadiliko yaja kuipa mamlaka kamili NEMC
“Jukumu la baraza ni kuhakikisha uzingatiaji na utekelezaji wa sheria na kanuni za mazingira unazingatiwa. Baraza limelenga kuwafikia wananchi na kuwapa elimu ya utunzaji wa mazingira kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, hivyo baraza linaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa juu ya masuala ya mazingira,” amesema Prof. Esnati Chaggu.
Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii NEMC, Lilian Lukambuzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NEMC ameeleza juhudi za baraza katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki inavyorahisisha utekelezaji wa majukumu ya baraza hali iliyorahisisha huduma kwa wadau wa mazingira.
SOMA: NEMC yatoa neno utunzaji bahari
Akiwasilisha wasifu wa Baraza la Mazingira, Dk Rose Salema amesema baraza katika utekelezaji wa majukumu yake linasimamia misingi ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Katika ziara hiyo iliyokuwa na timu ya watu 31 imehusisha watumishi kutoka Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Mamlaka ya Mazingira Zanzibar (ZEMA) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Shekha Mjaja Juma.
View this post on Instagram