Kamati ya kudumu ya Bunge Tamisemi yafunguka kituo cha afya Mtwara
MTWARA: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeishauri serikali kujenga nyumba za watumishi katika kituo cha afya cha mtandi kilichopo halmashauri ya mji Masasi mkoani Mtwara ili kurahisisha zaidi utoaji huduma kwa wananchi ambapo kimegharimu zaidi ya Sh milioni 500.
Wakizungumza leo Novemba 13, 2023 katika ziara ya siku moja ya kikazi kwa kamati hiyo inayofanyika kwa baadhi ya halmashauri mkoani humo ikiwemo halmashauri ya mji Masasi, Nanyamba mji pamoja na Newala wameeleza kuwa lengo la ziara hiyo kijiridhisha na hatua mbalimbali za utekelezaji wa miundombinu ya afya kwenye sekta hiyo kwenye halmashauri hizo.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba amesema hospitali lazima iwe na daktari wa dharura anayeishi jirani na kituo kutokana madaktari wote na wauguzi kuishi mtaani.
“Kwahiyo pamoja na mambo yote ambayo yanafanyika lakini lazima pawe na nyumba ya daktari pamoja na nesi wa dharura kipindi ambacho hospitali inaendelea kufanya kazi”amesema Makamba
Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Hajirath Mapembe amesema kituo kimeanza kutoa huduma mbalimbali Januari mwaka huu ikiwemo kwa wagonjwa wa nje (OPD), kliniki ya wajawazito na watoto pamoja na zingine.