Kamati yaridhishwa utekelezaji miradi

KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ikiwemo ya elimu iliyogharimu zaidi ya Sh milioni 800.

Akizungumza wakati kamati hiyo ya siasa mkoa wa Mtwara ilipotembelea miradi hiyo ya maendeleo ya sekta hiyo ya elimu kwa shule za msingi na sekondari kwenye halmashuri hiyo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Mobutu Malima amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

‘’Tumeridhika na utekelezaji wa Ilani, unakwenda vizuri chini ya Rais Samia Suluhu Hassan anayefanya kazi vizuri kwakweli tuna kila sababu ya kumuunga mkono na niwaombe mheshimiwa mkuu wa wilaya na timu yake wahikikishe wanakamilisha miradi hii kwa wakati kwa kuzingatia thamani ya fedha ya miradi inayotolewa’’amesema Mobutu.

Aidha katika ziara hiyo ya kutembelea miradi, kamati hiyo ya siasa imeongozana na sekretarieti ya mkoa huo na miongoni mwa miradi iliyotembelewa ikiwemo shule mpya ya sekondari ya kata ya Nalingu, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika shule ya msingi ya Ziwani na mingine.

Sambamba na hilo, Mobutu ameipongeza serikali kwa kuendedelea kusisitiza na kuhakikisha watoto wote wenye sifa wanakwenda shule ambapo mpaka sasa suala la usajili wa wanafunzi wanaoenda kuanza darasa la kwanza na darasa la awali katika maeneo yote waliyopita limefikia asilimia 80.

Amesema katika asilimia hiyo 80 ya usajili wa wanafunzi hao, asilimia 20 zilizobaki ametoa rai kwa viongozi hasa wa vijiji kuendelea kuwahimiza wazazi wawapeleke watoto mashuleni kwa ajili ya usajili na hatimaye waje shuleni kuanza masomo hayo.

‘’Naomba kutoa rai kwa waazi, kuendelea na jitihada za kuwalisha watoto katika shule kwa kutoa chakula asubuhi na mchana kwani iwe sehemu ya kivutio cha watoto kupenda kusoma’’amesisitiza.

Ameongeza kuwa, ‘’Vile vile nitoe rai kwa viongozi hasa wa kuchaguliwa kuendelea kuhamasisha wazazi umuhimu wa watoto kuwapeleka shule wakati wote kwasababu ndiyo rasilimali pekee ya kumrithisha mtoto’’

Mmoja wa wazazi kutoka kijiji cha Nalingu kwenye kata hiyo, Shem Yusufu ameipongeza serikali wa jitihada kubwa ya kuendelea kutilia mkazo suala la elimu kwani watazingatia maagizo yanayotolewa na serikali hiyo kuhusu kuwapeleka watoto shule.

Pia ameahidi kutorudi nyuma kwenye suala la elimu na badala yake shule zinapoenda kufunguliwa hivi karibuni watahakikisha watoto wanaenda shule na watachangia chakula.

Habari Zifananazo

Back to top button