Kampuni 100 zatarajiwa kushiriki maonesho ya famasia Dar

ZAIDI ya kampuni 100 zinatarajiwa kushiriki maonesho ya famasia maarufu kama ‘Pharmatech East Africa’ yanayorajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Agosti 30 hadi Septmba Mosi, mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Rais wa Chama cha Wafamasia nchini (PST), Fadhili Hezekiah wakati wa semina kwa wanahabari iliyofanyika leo, Ijumaa, jijini Dar es Salaam huku akisema hadi sasa kampuni 60 zimeshathibisha ushiriki wake katika onesho hilo.

“Maandalizi yameshakamilika maonesho haya ni mahususi na muhimu kama Taifa kuweza kujitokeza kujionea kujifunza kwani ni ya kwanza na ya kipekee kwa Tanzania hasa sekta ya afya. Tunategemea kuwa na makampuni zaidi ya 100 lakini hadi sasa tayari makampuni 60 yamethibitisha hii ni hatua kubwa sana kwetu kama waandaji kwa ushirikiano na kampuni ya ETSIPL,” Rais huyo ameeleza.

Amewataka wadau ikiwemo vyuo vya famasi nchini kujitokeza kwa wingi kujionea maonesho hayo kwani ni sehemu ambayo watajifunza na kupata mashirikiano.

‘’Makampuni yataonesha bidhaa zao ikiwemo dawa na vifaa tiba, tutaona dawa kuanzia hatu ya awali hadi inapokuja kuwa dawa…kutakuwa na vitu zaidi kutoka kwenye makampuni haya makubwa duniani, ikiwemo Bara la Ulaya, Asia na kwingine,”amesisitiza.

Naye Mtendaji Mkuu wa kampuni ya ETSIPL ya maonesho ya kibiashara kutoka India, Digvijay Singh amesema Tanzania imekuwa ya bahati kubwa, kwani makampuni makubwa yanakuja kuonesha bidhaa zao ambapo itachagiza fursa za uwekezaji.

‘’Kampuni kubwa kutoka nchi kama India, Uganda, Misri, Kenya, Rwanda na nyingine nyingi Bara la Ulaya, zinakuja kuonesha bidhaa zao, dawa na vifaa tiba…ambapo pia itakuwa ni fursa za wao kuwekeza hapa nchini, hivyo wadau na watu mbalimbali waje waone ni bure kabisa,’’ amesema Singh.

Aidha, maonesho hayo pia yanawezeshwa na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia Wizara ya Afya, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA], Bohari kuu ya Dawa [MSD] na wengine wengi.

Wakati huo huo, Rais wa Chama cha Wafamasia nchini (PST), Fadhili Hezekiah ameahidi kuwa kuweka mbele weledi na kutumia fursa zilizopo kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya wingi na bei rahisi nchini.

“Lakini katika nchi zinazoendelea kuna ufinyu wa matumizi ya wafamasi wapo wamiliki wa maduka wanaweka watu ambao hawakidhi vigezo…, wafamasia wanapaswa kuwa na shahada ya kwanza. Kuna wa diploma; hawa wanatofatiana kidogo kwenye majukumu,”amebainisha Fadhili.

Habari Zifananazo

Back to top button