BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema ujumbe wa watu 40 unaojumuisha wawakilishi wa kampuni za utalii za China utawasili nchini kesho.
Balozi Kairuki alilieleza HabariLEO kuwa ujumbe huo pia utajumuisha waandishi wa habari wa China na washawishi wa mitandao ya kijamii.
Alisema ubalozi huo kwa ufadhili wa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO) na Benki ya NMB wameandaa ziara hiyo ikijumuisha mawakala wa usafiri, waandishi wa habari na watu wenye ushawishi kutoka China kutembelea Tanzania kuanzia Mei 11 hadi Mei 23, mwaka huu.
Balozi Kairuki alisema ziara hiyo inaratibiwa kwa ushirikiano na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Kamisheni ya Utalii Zanzibar.
“Watakuja Tanzania kwa ziara ya takribani siku 10 kuanzia Mei 11 mwaka huu. Watatembelea Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam,” alisema na kuongeza:
“Ziara hii pia itajumuisha mawakala wa utalii kutoka kampuni zinazoongoza katika kusafirisha watalii nje ya China ikiwemo kampuni ya utalii ya China Tourism Group, CYTS na CAISSA.
“Vilevile ziara hii itajumuisha waandishi wa habari na wapiga picha kutoka vyombo vya habari vya China zikiwamo televisheni za majimbo ya Jiangsu na Guangdong yanayoongoza kwa uchumi mkubwa nchini China.”
Balozi Kairuki alisema ubalozi huo unatarajia kuvutia watalii wengi kutoka katika majimbo hayo mawili na kwamba lengo la ziara hiyo ni kuwaonesha vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Balozi Kairuki alisema wageni hao pia watakutana na wadau wa utalii wa Tanzania wakiwemo waongoza watalii, TTB na Kamisheni ya Utalii Zanzibar.
Alisema lengo la kuwakutanisha na wadau hao wa utalii ni kutoa fursa kwa ajili ya kujipanga kuanza kuitangaza Tanzania kwenye soko la China ili kuanza kuleta watalii kutoka soko la China.
Alisema takwimu za mwaka jana zinaonesha kuwa Jimbo la Jiangsu lilikuwa na idadi ya watu milioni 80 na pato la kila mtu lilikuwa Dola za Marekani 20,000.
Balozi Kairuki alisema Jimbo la Guandong lilikuwa na idadi ya watu milioni 126 na pato la kila mtu kwa Pato la Taifa lilikuwa Dola za Marekani 14,800.