Kanuni uchaguzi Naibu Meya, Naibu Wenyeviti zahojiwa

DODOMA. SERIKALI imesema ikipokea hoja kutoka kwa wadau walio wengi kuhusu hitaji la mabadiliko ya kanuni ya uchaguzi wa Naibu Meya na Naibu Wenyeviti wa Halmashauri itafanyia kazi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange kutokana na swali la Mbunge wa Viti Maalum, Janejelly Ntate, aliyehoji ni lini Serikali itarekebisha utaratibu wa Naibu Meya na Naibu Wenyeviti wa Halmashauri kuhudumu miaka mitano badala ya kuchaguliwa kila mwaka.

“Kanuni za Kudumu za Halmashauri za Wilaya zinazoelezea uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti zimetungwa chini ya kifungu cha 70(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 287 na Kanuni za Kudumu za Halmashauri za Miji zinazoelezea Uchaguzi wa Naibu Meya zimetungwa chini ya kifungu cha 42 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288.

‘Serikali inatambua kuwa, mabadiliko ya sheria, kanuni na taratibu ni sehemu muhimu ya utawala bora na maendeleo endelevu ya jamii. Hata hivyo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikipokea hoja kutoka kwa wadau walio wengi kuhusu hitaji la mabadiliko ya Kanuni hizi itafanyia kazi,” amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alisimama baada ya kipindi cha maswali na majibu akiomba muongozo wa Spika kuhusu suala hilo, kwamba ni vyema likaangaliwa vizuri kwani ukifanyika uchaguzi kila mwaka inakuwa ni vurugu badala yake iwe angalau miaka miwili na nusu.

Hata hivyo akijibu muongozo huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema kwa vile katika majibu serikali imesema kama wadau wana hoja wazipeleke, ni vyema wabunge kama wadau muhimu wana nafasi ya kufanya hivyo na kupitia pia kamati ambayo inasimamia TAMISEMI.

Habari Zifananazo

Back to top button