NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema mafanikio yanayoonekana sekta ya nishati ni jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kwani ndiye anayetafuta fedha za kutekeleza miradi ya nishati nchini.
Kapinga amesema hayo leo Novemba 07, bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Miradi mingi inatekelezeka kwa sababu ya jitihada za Mheshimiwa Rais, huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dk Doto Biteko akihakikisha kwamba miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na weledi mkubwa,” amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa sekta ya nishati ina umuhimu mkubwa nchini kwani ni sekta wezeshi katika kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia biashara, viwanda, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kijamii.
Kapinga amesema katika kipindi chote cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Sekta ya Nishati imejikita katika kuhakikisha inaboresha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na kuboresha misingi ya kiuchumi katika sekta ya mafuta na gesi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira wezeshi kwa kuhusisha sekta binafsi.
Amesisitiza kuwa wakati wa kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa mwaka 2021 nchi ilikuwa na megawati 1,571 za umeme kwenye gridi ya taifa lakini utakapokamilika mradi wa umeme wa Julius Nyerere nchi itakuwa na megawati 3,914.
Amesema mradi wa Julius Nyerere hivi sasa unazalisha megawati 940 kupitia mitambo minne na kuongeza kuwa ili kuwa na umeme mwingi zaidi serikali inaangalia vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme.
Kapinga ameongeza kuwa serikali inatekeleza miradi mingine ya uzalishai umeme ikiwemo Malagarasi 49.5 MW, Kakono 87.8 MW pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa jua wa Kishapu Shinyanga utakaozalisha meagawati 150 ambao ujenzi wake umeanza.
Ameeleza kuwa, serikali ya awamu ya sita inayo azma na nia ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme inaendelea.
Akizungumzia uzalishaji umeme kwa kutumia Jotoardhi, Kapinga amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na vyanzo vyenye uwezo kuzalisha takriban megawati 5,000 na kuongeza kuwa serikali ina ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi.
Amesema tayari maeneo matano yameshabainishwa kwa ajili ya kupata nishati ya jotoardhi ikiwemo Ruhoi, Natron, Mbozi, Songwe na Kiejo-Mbaka.
“Mheshimiwa Rais ametoa fedha takriban Sh bilioni 15.7 kwa ajili ya kununua mitambo ya uchorongaji maeneo haya ambayo tumeyabaini yana rasilimali ya jotoardhi,”amesema Kapinga
Kuhusu nishati jadidifu amesema mwelekeo wa serikali ni kuendeleza zaidi vyanzo vya nishati jadidifu ili kupunguza utegemezi wa kiuchumi, kuongeza usalama wa nishati na kuleta uendelevu wa kinishati ambao unachangia kiasi kikubwa katika kulinda mazingira.
Amesema pamoja na miradi ya uzalishaji umeme serikali pia inawekeza katika miradi mbalimbali ya usafirishaji umeme ya msongo mkubwa na mdogo ambapo baadhi ya miradi inayotekelezwa itaiunganisha Tanzania na nchi jirani.
Ameitaja baadhi ya miradi inayoiunganisha Tanzania na nchi jirani kuwa ni mradi utakaoiunganisha Tanzania na nchi nane za Ukanda wa Jangwa la Sahara pamoja na mradi unaoiunganisha Tanzania na nchi 14 za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Kapinga amesema mwaka 2021 serikali ilitoa takriban Sh trilioni 1.753 kuhakikisha umeme unapelekwa kwenye Vijiji vyote na vimebaki vijiji 78 kukamilisha vyote.