BANDARI ya Karema ni miongoni mwa bandari kuu ya kisasa katika ukanda wa maziwa makuu nchini iliyopo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Katavi ikiwa na umbali wa kilometa 120 kutoka mji wa Mpanda mkoani humo na kilomita 110 kutoka Barabara kuu ya Mpanda-Kigoma ambayo imejengwa kisasa kulinganisha na bandari nyingine za mwambao wa ziwa hilo.
Bandari hii ambayo ni miongoni mwa bandari 17 za Ziwa Tanganyika ina ukubwa wa eneo la heka 66 kwa jumla ikiwa na miundombinu ya kisasa kulinganisha na bandari nyingine za ziwa Tanganyika na ndiyo bandari pekee iliyo jirani zaidi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia bandari ya Kalemie ambayo ni bandari maarufu ya nchi hiyo.
Karema ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali yenye lengo la kufungua lango la biashara kati ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Tanzania lengo likiwa kupunguza utegemezi wa kulifikia soko kubwa la DRC kupitia nchi ya Zambia.
Mara kwa mara kumeshuhudiwa changamoto za vizuizi vya biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zinazopakana katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na hivyo kusababisha msongamano wa malori mipakani (Tunduma-Nakonde/Kasumbalesa) na kuathiri kasi ya uondoshaji shehena bandarini hasa Bandari ya Kuu ya Dar es salaam.
Mradi wa ujenzi wa uendelezaji wa Bandari ya Karema ni miongoni mwa miradi ya Kimkakati, inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Karema ni Mpango wa Serikali kuimarisha miundombinu ya Bandari na kuboresha utoaji wa huduma kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Ujenzi wa Bandari ya Karema ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020 na 2020-2025, Ibara ya 58, kifungu C. Aidha, Mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 (FYDP III), Ibara ya 5 (5.2.3) pamoja na mambo mengine, umeainisha kwamba ujenzi wa bandari hii ni muhimu ili kufungua lango la biashara kati ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Tanzania na hivyo kupunguza utegemezi wa kulifikia soko kubwa la DRC kupitia nchi nyingine (Zambia) ambako mara kwa mara kumeshuhudiwa changamoto za vizuizi vya biashara na hivyo kusababisha msongamano wa malori mipakani (Tunduma-Nakonde/Kasumbalesa) na kuathiri kasi ya uondoshaji shehena bandarini hasa Bandari ya Kuu ya Dar es salaam.
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Karema una manufaa makubwa katika Mkoa wa Katavi kwa kuwa utaongeza fursa za kiuchumi na kurahisisha zaidi usafiri wa abiria, usafirishaji wa mizigo pamoja na kuongeza ajira za moja kwa moja kwa wananchi wa Mkoa huo wenye utajiri mwingi wa malighali ya misitu, ardhi, mifugo na madini.
Kupitia bandari hii, Serikali imelenga kuwezesha wadau mbalimbali katika mnyororo wa biashara kunufaika na fursa za masoko ya bidhaa mbalimbali katika masoko ya nchi jirani na kuweka mazingira wezeshi kwa lengo la kuimarisha biashara na Taifa linufaike kikamilifu na masoko hayo.
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Karema ulianza kutekelezwa baada ya kusainiwa mkataba tarehe 13 Oktoba 2019 baina ya Serikali na mkandarasi kampuni ya ujenzi ya M/S Xiamen Ongoing Construction Group Company Limited kwa gharama ya Sh. Bilioni 47.97 ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 25 Oktoba 2019 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 25 Oktoba 2021 kwa muda wa miezi 24, lakini kutokana na changamoto za utekelezaji wa mradi, Mkandarasi aliongezewa muda wa miezi saba (7) hadi tarehe 20 Mei, 2022.
Mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema umehusisha ujenzi wa miundombinu katika kazi za ujenzi wa kidhibiti mawimbi yaani ‘breakwaters’, ujenzi wa maegesho ya meli ‘quaywall’, ujenzi wa eneo la kuhudumia meli ‘quay apron’ na ujenzi wa jengo la abiria ‘passengers lounge’.
Aidha, mradi pia umehusisha ujenzi wa ofisi za wadau wa Bandari, ujenzi wa ghala la kuhifadhi mizigo, ujenzi wa uzio yaani ‘security fence’, ujenzi wa yadi ya kuhifadhia mizigo mchanganyiko pamoja na makasha pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme, usalama na Tehama.
na kwa ujumla kazi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya Bandari hiyo zimekamilika kwa asilimia 99 kiwango ambacho kinaweza kutumika kwa mujibu wa mkataba.
Kwa sasa Mkandarasi anaendelea na kazi ndogo ndogo za kurekebisha dosari ambazo zilibainishwa wakati wa ukaguzi wa mwisho yaani ‘final inspection’ wakati wa kukabidhi mradi, ambazo kwa ujumla mkandarasi anatakiwa kuzikamilisha ndani ya kipindi cha uangalizi yaani ‘Defects Liability Period’ ambacho ni muda wa mwaka mmoja kuanzia Aprili 20, 2022 hadi Mei tarehe 19, Mei 2023.
Awamu ya pili ya utekelezaji wa bandari imehusisha ujenzi wa maegesho ya meli yenye urefu wa mita 150 na kina kisichopungua mita 4.5 ambacho ni mahususi kwa ajili ya kupokea meli zenye urefu wa hadi kufikia mita 75, upana wa mita 15 na kina (Draft) cha mita 3.5.
Pia ujenzi wa yadi yenye uwezo wa kuhifadhi makasha 1,500 kwa wakati mmoja yakipangwa mawili kwenda juu, ujenzi wa jengo la abiria, ghala la kuhifadhi mizigo lenye meta za mraba 2,000 na eneo la wazi ya kuhifadhia mizigo (open storage area) lenye ukubwa wa mita za mraba 22,500 kwa ajili ya mizigo mchanganyiko na makasha.
Sehemu nyingine ni uwekaji wa mizani yaani ‘weighbridge’ mbili kwa ajili ya kupimia mizigo inayoingia bandarini na mdaki yaani ‘scanner’ mmoja kwa ajili ya ukaguzi wa abiria.
Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula anasema bandari kwa sasa imekamilika kwa asilimia 100 na kwamba inachosubiri ni wadau tu (wafanyabiashara) kuanza kuitumia na kunufaika nayo.
“Wadau wa usafirishaji wa mizigo na abiria sasa waje tufanye biashara. Bandari imekamilika kwa asilimia mia moja na ina miundombinu yote ya kisasa na bora kabisa ukilinganisha na bandari nyingine zote katika ukanda huu wa ziwa Tanganyika. Bandari inawasubiri wao tu sasa waje waitumie,” Anasema Meneja MAbula na kuendelea,
“Tozo zetu ni rafiki kabisa sio za kuumiza kwa pande zote. Kubwa kabisa ni kwamba bandari hii ipo eneo la kimkakati kibiashara ambalo lipo katikati ya bandari zote za ziwa, lakini pia tupo jirani kabisa na Bandari ya Kalemie, iliyoko nchini DRC ambayo ni maarufu sana kwa kupitisha shehena kutoka Bandari za ziwa Tanganyika.”
Kuhusu manufaa ya kikanda mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema utaimarisha mahusiano ya kikanda kati ya Tanzania na nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo yatasaidia kuliingizia Taifa mapato na kuongeza ajira kwa wananchi.
“Bandari ni nzuri, imejengwa kisasa na hata kina chake ni kirefu, kwa kifupi inavutia sana. Changamoto ni barabara, kama Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara mapema wafanyabiashara wenzetu wengi wataleta boti zao.” Anasema Mussa Rashid ambaye ni mfanyabiashara wa kusafirisha mizigo kwa mashua wilaya.
Rashid aliipongeza Serikali kwa kujenga bandari hiyo katika eneo hilo la kimkakati na kusema imewarahisishia shughuli za usafirishaji wa bidhaa na mazao ya wananchi wa ukanda huo katika Wilaya ya Tanganyika.
Kwa sasa bandari ya Karema inapokea wastani wa boti mbili kwa mwezi za mizigo ambayo ni mazao ya kilimo na bidhaa nyingine kutoka vijiji vya Sibwesa, Ikola na vinginevyo vilivyopo ukanda wa ziwa hilo.
“Bandari hii ni miongoni mwa bandari bora kabisa zilizowahi kuengwa katika ukanda huu wa ziwa Tanganyika. Hapa tuna idara zote zinazotakiwa kuwepo katika bandari. Tuna idara ya uhamiaji, TRA, zimamoto, Afya na nyingine. Kama barabara ingekamilika mapema biashara ingekuwa nzuri zaidi kwa sababu hapa tupo jirani sana na wenzetu wa bandari ya Kalemie katika nchi ya Congo.” Anasema Ofisa Bandari ya Karema, Angetile Mwansasu.
Bandari ya Karema imejengwa katika eneo mahususi la kimkakati kwa ajili ya kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani za Kongo, Burundi na Zambia lakini lengo kuu hasa ni kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.
Bandari ya Karema ilianza kazi rasmi Septemba 1, 2022 ambapo wadau wa bandari kutoka TRA, Afya, Uhamiaji, TMA, Polisi wamekwishawasili bandarini na wanaendelea kutoa huduma.
Aidha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekwishaweka samani za ofisini pamoja na vitendea kazi muhimu vya kuhudumia shehena kama vile “mobile crane” yenye uwezo wa kunyanyua mzigo hadi tani 25, “forklifts” mbili, moja ikiwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani tano na nyingine ina uwezo wa kubeba tani tatu, Kompyuta za mezani (desktop) na printa mbili.
Mamlaka pia imeshapeleka wafanyakazi wanane ambao ni kutoka idara ya Utekelezaji (2), Fedha (1), Ulinzi (1), Uhandisi (3) na Zimamoto na Usalama (1) ili kuweza kutoa huduma kwa mizigo na abiria.