BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesema linataka kuyafanya mashindano ya Kombe la Dar Port Kagame kuwa makubwa zaidi kuanzia msimu ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Rais wa CECAFA Wallace Karia amesema baraza linafanya mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusu namna gani ya kuhakikisha michuano hiyo inafanyika kwa kiwango kikubwa.
Katika kuhakikisha yanapewa kipaumbe kikanda amehimiza vyama vya soka kila nchi kuyaingiza kwenye kalenda zao ili kila mwaka mwezi kama huu yawe yanafanyika kuzisaidia timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kujiweka imara.
SOMA: Vigezo ufunguzi, fainali Afcon 2027 vyatajwa
“Sisi tumeyaingiza kwenye kalenda yetu, nchi wanachama nazo zifanye hivyo ili timu zijiandae mapema kushiriki,”amesema Karia ambaye pia, ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Amesema mwakani mashindano hayo yataanzia hatua ya robo fainali kuzipa nafasi timu kujiandaa na mashindano mengine zikiwemo Ligi Kuu.
Amesisitiza pia kwamba mashindano mengine kadhaa yamepangwa katika ukanda huo mwishoni mwa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF ukanda wa CECAFA, kufuzu CECAFA ya CAF U-17, kufuzu CECAFA ya CAF U-20, kufuzu CECAFA shule za CAF na Ubingwa wa Wanawake CECAFA U-20.
Aliwashukuru wadhamini wa mashindano hayo msimu huu wakiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Mamlaka ya Bandari Tanzania(PTA) bandari ya Dar es Salaam akisema yamekuwa yenye ushindani.
akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, John Auka Gecheo, amevishukuru vyombo vya habari kwa kazi vinayofanya na kuwatia moyo kuendelea kuupa umuhimu unaostahili kwa mpira wa miguu katika ukanda wa CECAFA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa CECAFA, Ahmed Mgoyi, amesema kuwa hatua ya makundi ya Kombe la CECAFA Dar Port Kagame 2024 imeenda vizuri, lakini amewaomba mashabiki zaidi kujitokeza zaidi wakati hatua ya nusu fainali Julai 19 na fainali pamoja na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Julai 21.
Katika nusu fainali ya CECAFA, APR ya Rwanda itachuana na Al Hilal ya Sudani kwenye Uwanja wa KMC huku Al-Wadi ya Sudan ikitarajiwa kuikabili Red Arrows ya Zambia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.