DAR ES SALAAM; RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameweka wazi vigezo vitakavyotumika kuchagua nchi itakayoandaa sherehe za ufunguzi za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027.
Fainali hizo zitaandaliwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na moja kati ya hizo nchi itaandaa sherehe za ufunguzi za mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki.
Hivi karibuni msemaji wa serikali ya Kenya alisema nchi hiyo imechaguliwa kuandaa sherehe za ufunguzi za mashindano hayo mwaka 2027 na kuzua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Karia ambaye pia ni Rais wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), alisema Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) bado halijapanga sherehe za ufunguzi zitafanyika nchi gani.
Karia alienda mbali kwa kutaja vigezo vya nchi itakayopewa nafasi ya kuandaa sherehe hizo kuwa ni hamasa kubwa, mashabiki kuingia kwa wingi uwanjani kwenye michezo mbalimbali, amani na utulivu.
Aliwaomba waandishi wa habari kuhamasisha mashabiki wa soka wa Tanzania kuendelea kujitokeza uwanjani kwa wingi kila timu ya taifa inapocheza.
Soma pia:https://habarileo.co.tz/tujiandae-kwa-fursa-afcon-2027/
Karia alisema yeye ni Rais wa Cecafa na anaingia kwenye vikao vya utendaji vya Caf na kusisitiza shirikisho hilo la soka la Afrika halijakaa kuchagua nchi ya kuandaa sherehe za ufunguzi kwenye fainali hizo.
“Ingawa mimi ni Rais wa Cecafa lakini naingia kwenye Kamati ya Utendaji ya Caf, bado hatujatoa maamuzi,” alisema Karia.
Alisema taarifa iliyosambazwa na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Kenya haina ukweli na ina lengo la kujenga ushawishi wapewe nafasi hiyo.
Kauli hiyo ya Karia iliungwa mkono na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa aliyesema Caf bado haijakaa kufanya maamuzi wapi sherehe hizo za ufunguzi zitafanyika.