Kariakoo yavunja rekodi makusanyo kodi

Sehemu ya eneo la Kariakoo Dar es Salaam.

MKOA wa kikodi wa Kariakoo umevunja rekodi kwa kukusanya Sh bilioni 40.8 sawa na asilimia 102 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kwenye bonanza la michezo lililoandaliwa na TRA na wafanyabiashara wa Kariakoo kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete.

Kidata alisema mkoa wa kikodi wa Kariakoo wenye wafanyabiashara 30,000 umekusanya Sh bilioni 40.8 sawa na asilimia 102 kwa mwaka uliopita wa fedha 2022/2023 ambapo awali kabla Kariakoo haijawa mkoa wa kikodi walikuwa wakikusanya Sh bilioni 14 kwa mwaka.

Advertisement

“Kiasi hiki ni wastani wa Sh bilioni tatu kila mwezi na Kariakoo imeipita mikoa yote ya kikodi ambayo ni Tegeta, Kinondoni, Ilala na Temeke, kabla haijawa mkoa wa kikodi zilikuwa zinakusanywa Sh bilioni 14 kwa mwaka,” alisema Kidata.

Pia alisema Kariakoo ilifanywa mkoa wa kikodi Julai mwaka 2018 na inahudumia wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati na visiwa vya Comoro.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akizungumza na wanamichezo na wafanyakazi wa TRA, aliwataka kubuni mbinu nyingine ya namna ya kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara kama wanavyofanya kwa wafanyakazi wa serikali na wamiliki wa magari.

Pia Chalamila aliipongeza TRA kwa kuandaa bonanza hilo kwa kile alichoeleza linawaweka karibu na walipa kodi na kufanya ukusanyaji wa mapato kuwa wa kidiplomasia.

“Diplomasia ya ukusanyaji mapato inasaidia kuonekana kuwa TRA siyo chombo nyang’anyi, na niwaambie ukweli hakuna mtu atakayewapenda wakati mnapokusanya kodi ambazo zinakwenda kutumika kwenye miradi ya maendeleo.

“Cha msingi mnatakiwa kubuni njia ya kukusanya kodi kwa wafanyabiashara kama mnavyofanya kwenye magari na wafanyakazi wa serikali. Hata kanisani wachungaji siku hivi wanatulazimisha tutoe sadaka na niwaambie migomo siyo afya wakati serikali ikikusanya mapato na  haisaidii kwa sababu fedha hizo zinatumika kwenda kuwajengea miundombinu,” alisema.

Pia Chalamila alisema wapo kwenye vikao ili soko kuu la Kariakoo litakapomalizika wafanyabiashara wapewe leseni za kufanya biashara kwa saa 24 na mwendokasi zifanye kazi saa 24 ili kuendelea kupandisha uchumi wa Kariakoo na Dar es Salaam.

“Mfanyabiashara wa baa anafanya biashara saa 24 kwa nini na sisi wafanyabiashara wa Kariakoo wasifanye biashara saa 24 kwa sababu siku hizi mabasi yanasafiri saa 24 na mfanyabiashara akifika saa 5:00 usiku aende Kariakoo kufunga mzigo wake asubuhi aanze safari tena na kama wasiwasi ni usalama basi ni vizuri tujue panapovuja,” alisema Chalamila na kushangiliwa.

1 comments

Comments are closed.