Katambi azungumza na vijana fursa za ajira

NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, ametoa wito kwa vijana kote nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na wadau wa maendeleo ili kuboresha maisha yao.

Akizungumza leo katika hafla ya kugawa vifaa vya kilimo biashara kwa vijana wafanyabiashara wa Mkoa wa Iringa, Katambi amesisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau katika kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

Hafla hiyo iliyofanyika mjini Iringa, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Feed the Future Tanzania-Imarisha Sekta Binafsi, unaofadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID) katika mkoa wa Iringa na Mbeya.

Vijana 50 kutoka mkoa wa Iringa wamekabidhiwa vifaa mbalimbali vinavyowezesha kilimo bora na biashara endelevu katika juhudi za kuwainua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa kugawa vifaa hivyo, Naibu Waziri Katambi alisema, “Vijana ni asilimia 60 ya nguvu kazi ya taifa. Hivyo ni muhimu watambue nafasi yao na kutumia vyema fursa kama hizi zinazotolewa na serikali na wadau wa maendeleo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.”

Kwa upande wake, mwakilishi wa USAID, Eric Johnson, alisema msaada huo ni matunda ya ushirikiano wa muda mrefu baina ya Marekani na Tanzania, unaolenga kuendelea kufungua fursa za maendeleo kwa vijana.

“Tunatambua uwezo mkubwa wa vijana wa Tanzania na tumejipanga kuwa sehemu ya safari yao ya mafanikio,” aliongeza Johnson.

Mradi huo wa miaka mitano ambao uko wa pili wa utekelezaji wake unalenga kuwafikia vijana 30,000 nchini na kutengeneza ajira zaidi ya 5,000.

Mradi huo si tu unawasaidia vijana kupata vifaa vya kilimo biashara, bali pia unawapatia mafunzo ya biashara, kuwahusisha na taasisi za kifedha, kuwapatia mitaji, na kuwatafutia masoko.

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Yasinta Migodela kutoka kijiji cha Igingilanyi, Iringa. Yasinta amefanikiwa kuanzisha kampuni ya Yami Avocado Enterprises inayojishughulisha na utengenezaji wa viungo vya chakula na unga wa lishe baada ya kupatiwa msaada wa mashine, mzani, na vifungashio.

“Mradi huu umenisaidia kufikia ndoto zangu na kubadilisha maisha yangu kwa njia isiyowezekana,” alisema Yasinta kwa furaha.

Method Nyika, kijana mwingine aliyenufaika na mradi huu, ameanzisha kiwanda cha kusindika unga wa sembe katika eneo la Viwengi, wilayani Kilolo.

Kwa msaada wa vifaa na mafunzo aliyoyapata, ameweza kupanua biashara yake na kutoa ajira kwa vijana wengine.

Kwa ujumla, Feed the Future Tanzania inatoa mwanga mpya kwa vijana nchini, ikiwasaidia kutengeneza mustakabali bora kupitia kilimo na biashara, huku ikichochea ukuaji wa sekta binafsi nchini..

Habari Zifananazo

Back to top button