Katekista kortini akidaiwa kumbaka mwanafunzi

MKAZI wa Mlangali wilayani Ludewa, mkoani Njombe, Simon Njavike (43) ambaye pia ni katekista wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mlangali amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya hiyo akidaiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 17.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa, Isaac Ayengo, Mwendesha mashitaka, Angelo Marco alieleza kuwa mshitakiwa huyo ni mwalimu wa watoto wa kipaimara.

Marco aliieleza mahakama kuwa binti huyo ni mmoja wa wanafunzi hao na amekuwa akifanya vizuri katika mafunzo hayo hivyo mshitakiwa alimpa Sh 10,000 kama zawadi ya kufanya vizuri kwenye mafunzo.

Ilidaiwa kuwa baada ya siku kadhaa mshitakiwa huyo alianza kumtaka kimapenzi binti huyo ambaye alikataa na ndipo akataka arudishiwe Sh 10,000 yake lakini binti alishindwa kuirudisha kwa kuwa hakuwa na fedha hizo.

Marco alidai kuwa baada ya siku kadhaa Njavike alimuita binti huyo nyuma ya kanisa majira ya mchana ambako kuna msitu na msichana alipofika akamkamata kwa nguvu na kuingia naye katika msitu huo kisha akatimiza lengo lake hilo na kutokomea kusiko julikana.

Mahakama ilielezwa kuwa Jeshi la Polisi lilifanya jitihada za kumtafuta na baada ya siku kadhaa alikamatwa. Kesi hiyo imeahirishwa mpaka itakapotajwa tena Februari 9, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button