Katimba awatoa hofu wanafunzi Uyui

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Zainabu Katimba.
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Zainabu Katimba amewatoa hofu wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lolangulu iliyopo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora ambao walikumbwa na janga la moto kuwa serikali itasaidia  kurejesha miundombinu.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo leo Katimba amesema baada ya kupokea taarifa ya tathmini ya uharibifu uliotokea wataangalia namna ya kurejesha miundombinu hiyo.
“Sisi kama Ofisi ya Rais-TAMISEMI na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba niwaambie tu tunatambua adha kubwa ambayo mnakutana nayo. Sasa miundombinu yetu ndiyo kama hivi imepata changamoto nataka niwahakikishie kwamba tunasubiri ripoti ya tathmini ya kina.
“Na sisi kama Ofisi ya Rais Tamisemia tutashirikiana nanyi kuona namna gani tunaweza kuwaunga mkono katika janga hili ambalo mmelipata la uharibifu wa miundombinu ya darasa ambalo imetokana na moto, hivyo ujio wangu utakuwa na faida,”amesema Katimba.
Ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama na wazazi ambao wamesaidia kuzima moto na kuokoa mali za umma zisiendelee kuteketea zaidi wakati wa janga hilo.
Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lolangulu, Justine Machage amesema katika tukio hilo hakuna mwanafunzi aliyepata madhara ya kujeruhiwa au kupoteza maisha na chanzo chake hakijabainika.
Amesema vifaa vilivyoteketea ni darasa lenye thamani ya Sh milioni 26, magororo 30 ya wanafunzi wa kidato cha pili na nne ya wavulana, ndoo za kuogea, sare za shule, vitabu, daftari, mabegi ya nguo na masanduku ya kutunzia vifaa vya wanafunzi (trunke).
Awali, Diwadi wa Kata ya Ilolangula Mohamedi Linso amesema baada ya taarifa za moto kuenea wananchi walikusanyika na kuunganisha nguvu za kudhibiti moto uliokuwa unazidi kwa kuvunja ukuta wa vyumba ili kuzie usiendee kwenye vyumba.

Kwa mujibu wa takwimu za mkoa wa Tabora mkoa huo wenye wilaya 7 na Halmashauri za wilaya 8 una shule za sekondari 153 na za msingi 671.