MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwasa amewataka wakuu wa wilaya za mkoa huo kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye sekta ya elimu ili kuhakikisha walimu wanafanya kazi zao ipasavyo na mkoa huo unapiga hatua katika elimu.
Mwasa alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa vitabu vya miongozo ngazi ya mkoa vilivyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) vikiwa na lengo la kuboresha elimu kwa ngazi ya msingi na sekondari.
Alisema serikali mwaka wa fedha 2021/2022 imetumia zaidi ya Sh bilioni 38 kwenye sekta ya elimu kwa Morogoro ili kuboresha miundombinu ya kujifunza na kujifunzia kwa lengo la kuboresha elimu.
Mwasa alisema iwapo wanafunzi watafundishwa vizuri na kufaulu mitihani yao na walimu kusimamia miongozo iliyoko kwenye vitabu hivyo ipasavyo mkoa huo utapiga hatua mbele katika sekta ya elimu.
Pia aliwaagiza viongozi ndani ya mkoa huo hususani walimu kuhakikisha wanaandikisha kila mtoto pindi muda huo utakapofika , huku akisisitiza watoto kutoka jamii ya wafugaji kutoachwa hata mmoja kwenye uandikishwaji huo.
“Niwakumbushe kwamba elimu ni haki ya kila mtoto, hata yule ambaye amezaliwa, wazazi wake hawajatilia umuhimu wa elimu sisi viongozi wa serikali mkiwemo ninyi walimu mnawajibika kuhakikisha watoto wote wanapata slimu,” alisema.
Naye Ofisa Elimu Mkoa huo, Germana Mung’aho alisema miongozo hiyo mitatu inakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na kuwa nyenzo muhimu kwa walimu katika kufanyia kazi ili kuboresha elimu ndani ya mkoa huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando alisema atakuwa mstari wa mbele maeneo ya kazi kutekeleza maagizo ya mkuu wa mkoa kwa kasi inayotegemewa na kiongozi wao.
Uzinduzi wa vitabu hivyo vya miongozo ngazi ya taifa ulifanyika mkoani Tabora Agosti 4 mwaka huu na Waziri mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA, mojawapo ya miongozo hiyo ni “Mkakati wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji ngazi ya Elimu Msingi”.
Miongozo mingine ni pamoja na “Changamoto katika uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari, nini kifanyike?” na “Mwongozo wa Uteuzi wa Viongozi wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa”.