Kaya 38,217 Kagera kufikiwa Bima ya Afya kwa Wote

KAGERA: Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, amezindua awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi, hususan kaya zenye uhitaji, makundi maalumu, vikundi vya ushirika na jamii kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kanali Kido amesema jumla ya kaya 38,217 zenye wakazi 84,934 zinatarajiwa kusajiliwa katika awamu hiyo ili kunufaika na huduma za matibabu kupitia mpango huo.
Amesema kaya maskini zinazotambuliwa rasmi zitasajiliwa na Serikali bila kuchangia fedha, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Aidha, amesema kaya nyingine, vikundi na vyama vya ushirika vitachangia Sh 150,000 kwa mwaka, huku kifurushi husika kikitarajiwa kuwezesha watu sita kupata huduma za matibabu.
Mkuu huyo wa mkoa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha usajili na utambuzi wa wanufaika unafanyika hadi katika ngazi za vijiji na mitaa ili wananchi wote wanaostahili wapate fursa ya kujiunga na mpango huo.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali, watendaji wa maeneo husika na wadau wengine ni muhimu katika kutoa elimu na taarifa sahihi kuhusu mpango huo na namna wananchi wanavyoweza kunufaika nao.
Kwa upande wake, Meneja wa NHIF, Ismail Kangeta, amesema katika awamu ya kwanza ya usajili wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Kagera, kaya 15,284 zenye wakazi 67,451 zilisajiliwa.

Amesema mafanikio hayo yanaweka msingi wa kuendeleza usajili katika awamu ya pili, huku mfuko huo ukiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuongeza mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya.

Kangeta ameeleza kuwa mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima na kupunguza changamoto za gharama wanapohitaji huduma hizo.
Kaulimbiu ya mpango huo ni: “Bima ya Afya kwa Wote kwa Uhakika wa Matibabu.”



