KAZI kubwa aliyoifanya akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Afya na Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imemuwezesha Benito Kayugwa kupata alama za juu kukwea madaraka baada ya leo kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Kayugwa ambaye ni diwani wa Kata ya Migoli, anafahamika kwa uwezo wake mkubwa wa kusimamia miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji diwani huyo ameonesha uwezo wa kuleta umoja kati ya wataalamu na viongozi, akihimiza mawasiliano bora ili kufanikisha utekelezaji wa miradi.
Licha ya majukumu ya kisiasa Kayugwa amekuwa akisisitiza umuhimu wa viongozi kuheshimiana na kufanya kazi kwa uadilifu bila kuingiza siasa katika masuala ya kiutendaji.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, amempongeza Kayugwa kwa kuchaguliwa kuwa msaidizi wake akisema ni kiongozi anayejali maendeleo na maslahi ya wananchi.
Wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamemchagua kwa kura zote 33 zilizopigwa kuwa makamu mwenyekiti wa halamashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi Kayugwa amewashukru madiwani wenzake na kuahidi kutoa mchango wake kwa kumsaidia mwenyekiti wa halmashauri kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
“Leo ni siku ya historia kwangu kwa imani kubwa mliyonipa waheshimiwa madiwani kuwa msaidizi wa mwenyekiti wetu, naahidi ntakuwa msaidizi mzuri wa mwenyekiti na sina maeneo mengi tutakutana kazini,” alisema.
Nao baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamempongeza Kayugwa kwa ushindi mnono wakimtaka kusimamia maslahi ya wananchi katika halmashauri hiyo.
SOMA:
Kupitia kikao hicho pia madiwani wamewasisitiza wataalam wa halmshauri katika sekta mbalimbali kuendelea kuwajibika ipasavyo katika utatuzi wa changamoto ili kuwapunguzia mzigo wa kujieleza kwa wananchi.
Miongoni mwa changamoto walizotaka ziangaziwe kwa ukaribu ni ukarabati wa miundombinu ya barabara hasa kipindi hiki ambacho mvua za masika zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali
Katika kikao hicho baraza hilo pia limeteua wajumbe na kuchagua wenyeviti wa kamati tano za kudumu ndani ya baraza hilo ambao watahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.