KISOZI, Uganda: NCHI za Kenya na Uganda zimeafikiana kutatua mgogoro wa uingizaji wa petroli katika nchi hizo kwa namna ambayo itahakikisha kunakuwa na bei ya ushindani zaidi na ufanisi wa juu zaidi wa vifaa.
Maafikiano hayo yamefanyika kati ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais wa Kenya, William Ruto, shambani kwa Rais Museveni katika Jimbo la Kisozi.
“Katika mkutano wangu na Rais @KagutaMuseveni leo, pia tulijadili haja ya nchi hizo mbili kufuatilia kwa haraka usanifu na ujenzi wa bomba la bidhaa iliyosafishwa ya mafuta ya petroli Eldoret-Kampala-Kigali.” Ameandika Rais Ruto katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mvutano baina ya Uganda na Kenya juu ya uagizaji wa mafuta ya petroli wakati Uganda ikifikiria kuagiza shehena yake yote kupitia bandari ya Tanzania badala ya Kenya.