Kheri James apokelewa kwa shangwe Iringa, awaapisha Ma-DC wapya

IRINGA: MKUU wa Wilaya mpya wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amepokelewa kwa heshima na shangwe katika ofisi ya mkuu wa mkoa huo, akiahidi kuitumikia Iringa kwa moyo, weledi na nguvu zake zote, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana hiyo ya kiuongozi.
Katika hafla hiyo maalumu ya mapokezi, ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, dini, vyama vya siasa na wananchi, RC James aliwaapisha rasmi wakuu wapya wa wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta na Kilolo Estomin Kyando — huku akiwataka kuwa viongozi makini, waaminifu na watakaosimamia kwa ukaribu maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
“Wito wangu kwa wakuu wa wilaya ni kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa kuzingatia sheria, mipango ya serikali na maadili ya utumishi wa umma,” alisisitiza James.
Akizungumza kwa hisia na heshima kubwa, RC James alisema uteuzi wake ni heshima ya kipekee kutoka kwa Rais, na akaahidi kutumia nafasi hiyo kwa kuhakikisha Iringa inasonga mbele kwa kasi zaidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aliahidi kuipa msukumo maalum sekta ya utalii, akieleza kuwa Iringa ni kitovu cha utalii kwa Kanda ya Kusini na hivyo kunahitajika mikakati ya makusudi ya kuendeleza vivutio vilivyopo na kuimarisha mazingira rafiki kwa uwekezaji katika sekta hiyo.
“Utalii una mchango mkubwa katika kutoa ajira, kuongeza mapato ya halmashauri na kuchochea shughuli za kiuchumi. Ni lazima tuweke mazingira bora kwa wawekezaji na kuhakikisha vipaumbele vinavyohusu sekta hii vinapewa uzito wa kipekee,” alisema.
Aliwahakikishia wananchi kuwa ataendeleza ushirikiano na wadau wote, akitumia uzoefu alioupata alipokuwa Mkuu wa Wilaya, kabla ya kupandishwa cheo kuwa Mkuu wa Mkoa.
Kuhusu maonesho ya utalii ya Karibu Kusini, James alisema atahakikisha yanaendelezwa kwa ubunifu na kwa namna isiyozuia juhudi za waandaaji, huku yakibeba matarajio ya kimkakati ya kuinua uchumi wa Iringa.