Kheri James apongeza mageuzi Mahakama Kuu Iringa

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameisifu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kwa mageuzi makubwa iliyofanya katika miaka 20 ya utoaji haki tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, akisema hatua hizo zimeongeza kwa kiasi kikubwa imani ya wananchi katika mhimili wa mahakama.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, RC Kheri alisema miaka 20 ya Mahakama Kuu Iringa ni safari ya mafanikio, ustahimilivu na mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa na Taifa.
Alisema Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imeleta maboresho makubwa yanayoonekana katika sekta ya utoaji haki, kuanzia uboreshaji wa miundombinu ya majengo ya Mahakama, ongezeko la Majaji na watumishi, matumizi ya TEHAMA katika kusikiliza na kuendesha mashauri, pamoja na kuongezeka kwa uaminifu wa wananchi katika mfumo wa utoaji haki.

RC Kheri aliongeza kuwa kuanzishwa kwa Kanda ya Iringa kulilenga kupunguza mlundikano wa mashauri katika kanda nyingine na kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi wa Iringa, Njombe na maeneo ya jirani.
Alisema hatua hiyo imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi na kuharakisha upatikanaji wa haki.
Akizungumzia ushirikiano kati ya Serikali na Mahakama, Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali imeendelea kuimarisha mahusiano hayo kama sehemu ya kusimamia misingi ya utawala bora.
Alitaja maeneo ya ushirikiano kuwa ni pamoja na kuboresha usalama wa majengo ya Mahakama, utoaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo, utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu sheria, pamoja na jitihada za pamoja katika mapambano dhidi ya rushwa.

Alisema ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Mahakama unawasaidia wananchi moja kwa moja kwa kuwa unajenga mfumo imara wa haki na kuimarisha uaminifu katika taasisi za umma.
RC Kheri alizungumzia pia mchango wa Mahakama katika maendeleo ya kiuchumi, akisema uwepo wa Mahakama Kuu Iringa umeongeza imani ya wawekezaji, kupunguza migogoro ya kijamii na kuongeza ufanisi katika mashauri ya ardhi, biashara na jinai.
Alisisitiza kuwa hakuna maendeleo ya kiuchumi bila amani na misingi ya haki, na Mahakama ndiyo nguzo inayolinda misingi hiyo.
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa tarehe 15 Desemba 2025, RC Kheri alisema shughuli mbalimbali zimeandaliwa.
Shughuli hizo zinahusisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu huduma za Mahakama, masuala ya mirathi, uandishi wa wosia, usuluhishi wa migogoro (ADR), haki za watoto, ndoa na talaka, pamoja na matumizi ya TEHAMA katika mashauri.
Aidha, kutafanyika mdahalo maalum katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), matembezi ya maadhimisho na kufungwa kwa wiki ya elimu kwa umma.
Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Desemba 15, 2025, ambapo RC Kheri amewataka watumishi wa Mahakama na wadau wa sheria kuendelea kutambua umuhimu wa haki kupatikana kwa wakati.
Alisema haki inapopatikana kwa wakati, imani ya wananchi huongezeka, na imani hiyo ndiyo msingi wa uchumi na ustawi wa jamii.



