Kibaha yapongezwa kuongoza kimapato

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa kuongoza kimapato kwa mwaka 2022/2023.

Kunenge alitoa pongezi hizo juzi katika kikao cha baraza maalumu la kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

“Upande wa asilimia mliongoza sio jambo dogo kwa halmashauri ya Wilaya kuongoza nchi nzima, mnastahili pongezi kwa juhudi mlizoonesha,” alisema Kunenge.

Alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Butamo Ndalahwa kwa kuendelea kuaminiwa na Rais na kuwatumikia wakazi wa Kibaha kwani utendaji na juhudi zake za kuwatumikia wana Kibaha zinaonekana.

Kunenge alisema anatambua kuna malimbikizo ya madeni ya wastaafu lakini halmashauri imefanya jitihada za kulipa malimbikizo hayo na juhudi zinaendelea za kulipa madeni hayo kadri fedha zinavyopatikana.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi na kuwataka wakuu wa idara kuhakikisha hawazalishi hoja.

Nickson aliwataka madiwani kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo katika kata zao ili kuepuka kuzalisha hoja za ukaguzi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanajibu hoja za mkaguzi wa ndani ipasavyo kwani hoja za CAG asilimia kubwa zinatokana na hoja za mkaguzi wa ndani.

Habari Zifananazo

Back to top button