Kigogo Polisi matatani kuachia watuhumiwa 19

JESHI la Polisi mkoani Tanga limemkamata ofisa wake anayedaiwa kuwaachia huru watuhumiwa wa uhujumu uchumi waliokamatwa na mali za magendo zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.2.

Mkuu wa Mkoa Tanga, Omary Mgumba amesema Septemba 8, mwaka huu akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa walikamata jahazi lililobeba mabelo 170 ya vitenge vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 570.

Mgumba alisema watu wanane walikamatwa wakituhumiwa kuhusika kwenye usafirishaji huo na walifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Duga wilayani Mkinga.

Advertisement

Alisema hayo alipotoa taarifa baada ya ziara kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya serikali na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ya hatua zilizochukuliwa kwa watuhumiwa 24 waliokamatwa na magendo ya vitenge wiki mbili zilizopita.

Mgumba alisema Septemba 11, kamati hiyo pia iliwakamata watu 20 na malori mawili aina ya Fuso yakiwa na mabelo 90 za vitenge kila moja.

Alisema watuhumiwa 14 kati ya hao walikuwa wabebaji, madereva wawili, makondakta wawili na wenye mali wawili na wote waliwekwa rumande kwa ajili ya hatua za kisheria.

Mgumba alisema alishangazwa kuona watuhumiwa wanne waliokamatwa na jahazi wameachiwa huru bila ya taarifa na hawakufunguliwa jalada la kesi kama vile hakuna kitu kilichofanyika.

Alisema pia watuhumiwa 15 kati ya 20 ambao walikamatwa na mabelo 180 ya vitenge, nao wameachiwa huru, lakini wamefunguliwa kesi za uhujumu uchumi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za kisheria.

“Nashangazwa na hiki kilichotokea cha kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao 19 kati 24 wa uhujumu uchumi na ukiuliza hakuna anaejua hili jambo sio la kawaida,” alisema mkuu wa mkoa.

Aidha, alisema alipofanya kikao na kamati hiyo alibaini kuwa Ofisa Upelelezi Wilaya ya Mkinga ndiye aliyehusika na kuachiliwa kwa watuhumiwa hao akidai alipewa maelekezo na Ofisa Upelelezi wa Mkoa ambaye hakuwepo katika kikao hicho.

Mgumba alisema haiwezekani Ofisa Upelelezi wa Mkoa aende kinyume na Kamanda wa Polisi Mkoa na kufanya hivyo kilichotokea ni sawa na hujuma na hakuna ushirikiano katika Jeshi la Polisi jambo linaloweza kuzorotesha mapambano ya uzuiaji wa biashara za magendo mkoani humo.

“Sasa Ofisa Upelelezi Wilaya akiulizwa hawa watuhumiwa vigezo gani vimetumika kuachiwa huru, anadai amepewa maelekezo na Ofisa Upelelezi Mkoa, hii ni sabotage! (hujuma),” alisema Mgumba.

Alisema ofisa huyo wa upelelezi wa wilaya yupo ndani na sheria itafuata mkondo wake.

“Nimshukuru Kamanda Polisi Mkoa Tanga, Safia Jongo baada ya kuona yametokea makosa, haraka alianza kuchukua maamuzi ya kumweka afisa huyo ndani huku hatua nyingine za kisheria zikifuatwa,” alisema.

Aliongeza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ikataa kujadili kilichotokea na kutoa taarifa kwa viongozi wa ngazi za juu kwa maelekezo zaidi kuhusu watumishi watakaobainika kuhusika.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, Specioza Owure alisema walikamata mali hizo za magendo na baadhi ya mabelo yamehifadhiwa katika ghala la mpaka wa Horohoro na bandarini Tanga.