Kigoma kuendeleza mpango nishati safi

WANANCHI wa Mkoa Kigoma wanatarajia kupokea mitungi 19,530 ya gesi safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mhandisi Mwandamizi wa Wakala wa nishati Vijijini (REA), Deusdedit Malulu amesema hayo akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Kigoma,  Thobias Andengenye alipofika ofisi kwa mkuu huyo wa mkoa kutoa taarifa kuhusu uwepo wa mpango huo ambapo amesema kuwa mpango huo unahusisha mitungi midogo ya ujazo wa kilo sita.

Malulu amesema kuwa serikali imeweka ruzuku kwenye mitungi hiyo hivyo kila mtungi ulio kamili utauzwa kwa shilingi 20,000 badala ya shilingi 40,000 baada ya serikali kuweka ruzuku ambapo kwa nchi nzima kiasi cha mitungi 400,000 inatarajia kuuzwa kwa gharama nafuu kuchochea matumizi ya nishati safi.

Advertisement

Mhandisi Malulu ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi REA amesema kuwa ili mwananchi anunue mtungi kwa gharama nafuu anapaswa kuwa na kitambulisho cha mpiga kura au kitambulisho cha Taifa na Kwamba ambaye hana vitambulisho hivyo hatafaidika na huduma hiyo.

Akizungumzia kutekelezwa kwa mpango huo mkoani Kigoma Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa mpango ni mzuri kutokana na kuunga mkono serikali kuchochea matumizi ya nishati safi sambamba na katika kupambana na uharibifu wa mazingira.

Andengenye amesema kuwa ni Imani yake kwamba baada ya mitungi hiyo ni wazi wananchi watakaotangulia watakuwa mashahidi wa mpango huo kuona matumizi ya nishati safi inavyoweza kudhibiti matumizi ya kuni na mkaa ambavyo vimekuwa na athari kubwa kimazingira na afya za watu na kwamba mkoa utachochea na kufanya uhamasishaji wa nishati hiyo.