Kigoma kupatiwa gari za wagonjwa 17

Mkoa wa Kigoma unatarajia kupata magari ya kubebea wagonjwa 17 yatakayosaidia kutatua changamoto ya huduma za rufaa pamoja na kupunguza vifo vya mama na mtoto katika mkoa huo.
Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel amesema hayo wakati wa ziara yake mkoani humo ambapo alikagua hali ya utoaji huduma na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kigoma.
Akifafanua alisema jumla ya magari ya wagonjwa yaliyonunuliwa na serikali ni 727 ambayo inatarajia kugawa nchi nzima, kila halmashauri itapata magari mawili na hospitali ya mkoa kupata gari moja kama njia ya kupunguza changamoto ya uhaba wa magari hayo mikoani.
“Tumenunua Ambulance 727, na tayari ambulance hizo zimeanza kuingia, na tumekubaliana angalau zifike ambulance 200, kuna uwezekano wa kila halmashauri kupata ambulance mbili na kila hospitali ya mkoa kupata ambulance, hivyo kuna uwezekano wa mkoa wa Kigoma kupata ambulance 17 zitazosaidia kupiga hatua katika huduma za Afya.” Amesema.
Aidha, Dk Mollel amewapongeza watoa huduma wa hospitali ya rufaa ya mkoa Maweni kwa jitihada na ubunifu wanaoendelea kuonesha katika kuboresha huduma kwa wananchi akisema imesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa ndani kwa zaidi ya asilimia 28 ndani ya muda mfupi, huku malengo yakiwa kupunguza asilimia zaidi ya 90.
Kwa upande mwingine naibu Waziri huyo amewataka viongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanakuwa na Washitiri wazuri na wenye lengo la kuwasaidia wananchi kwa kufuata vigezo na taratibu zote ili kuhakikisha hakuna changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vyote vya kutolea huduma.
imeendelea kupokea wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi ikiwemo nchi ya Burundi wanaofika kupata huduma kupitia hospitali hiyo ya Maweni.