Kigoma yapokea vyandarua milioni 1.7 kujikinga malaria

KIGOMA: Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye amesema kuwa Mkoa wa Kigoma umepokea vyandarua zaidi ya milioni 1.7 vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 10 ambavyo vinavyotarajia kugawiwa bure kwa wananchi ikiwa ni awamu ya kwanza ya mpango wa kuondoa malaria mkoani humo.
Andengenye amesema kuwa hayo wakati wa uzinduzi wa ugawaji huo wa vyandarua uliofanyika kimkoa katika Zahanati ya Rusimbi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo amesema kutolewa kwa vyandarua hivyo kuna mchango mkubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma aliitaka jamii ya Kigoma iache mila potofu kuwa vyandarua hivyo vinasababisha ukosefu wa nguvu za kiume na wanawake kushindwa kubeba ujauzito huku akiwaonya wale wanaotumia vyandarua hivyo kuvulia samaki na matumizi mengine ambayo si sahihi na kwamba hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.

Awali Mkurugenzi wa Ugavi kutoka Bohari ya Dawa nchini (MSD),Victor Sungusia alisema kuwa zaidi ya vyandarua milioni 60 vyenye thamani ya Sh bilioni 450 vimegawiwa kwa watanzania nchini kote ikiwa ni kutekeleza mpango wa serikali wa kukabiliana na kuondoa ugonjwa wa malaria nchini maarufu kama ziro malaria.
SOMA ZAIDI: Serikali kugawa vyandarau bila malipo Shinyanga – HabariLeo
Sungusia alisema kuwa pamoja na ugawaji wa vyandarua pia dawa za kupulia viua dudu pia zilitolewa ambapo mpango huo unalenga kuondoa malaria ili kuwafanya Watanzania kujikita kwenye shughuli za uzalishaji badala ya kusumbuliwa na ugonjwa huo kila wakati.

Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Kigoma waliojitokeza katika uzinduzi huo akiwemo Mwasiti himidi ambaye alipokea vyandarua alimshukuru Rais Samia kwa moyo wa upendo ambao umemsukuma kuhakikisha wananchi wake hawasumbuliwi na ugonjwa huo ili wajikite kwenye kufanya kazi na kwamba vyandarua hivyo vitawasaidia kuepukana na ugonjwa huo.
Naye Ramadhani Hussein alisema kuwa amejitolea kuwa mjumbe mzuri kwa wananchi kuwaambia watumie vyandarua hivyo vya kuzuia mambukizi ya ugonjwa wa malaria na kutokwenda kufanyia shughuli nyingine ambazo ni tofauti na malengo ya serikali kwani imewekeza fedha nyingi kulinda afya za wananchi wake.



