Kila la heri Simba, Watanzania wako nyuma yenu

SIMBA ina kila sababu ya kushinda Kombe la Shirikisho Afrika kwenye ardhi yake ya nyumbani.

Baada ya zaidi ya miaka 30 kulikosa kombe hilo Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru), Simba imepata fursa nyingine ya kushinda ubingwa huo nyumbani.

Safari hii haitakuwa Dar es Salaam kama ilivyokuwa mwaka 1993 waliposhuhudia taji hilo likitwaliwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast, itakuwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, Zanzibar.

Kwenye mechi ya kwanza ya fainali iliyofanyika Morocco, Mei 17, Berkane ilishinda mabao 2-0 na hivyo Simba itatakiwa kushinda mabao 3-0 Jumapili kushinda ubingwa huo.

Kuelekea mchezo huu wa marudiano wa Jumapili kumekuwa na shinikizo kubwa la nje ya uwanja kwa upande wa Simba hasa baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuutangaza Uwanja wa New Amaan Complex kutumika kwa ajili ya fainali hiyo.

Shinikizo hilo linaweza kuwa na athari hasi kwa upande wa Simba hasa kutokana na shauku yao ya kuona wanacheza mbele ya mashabiki wao Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambao wamekuwa wakipata matokeo mazuri hasa linapokuja suala la mechi za kimataifa.

Tunaona shauku hiyo ya Simba lakini tunaamini wao ni timu kubwa yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na mazingira ya namna hiyo na hivyo kupata matokeo mazuri.

Simba imewahi kuwa kwenye mazingira mengi magumu kama ya namna hii lakini kutokana na ukomavu wao hasa linapokuja suala la mechi za kimataifa, wamekuwa wakipata matokeo mazuri.

Tunaamini, hata kwenye mchezo wa kesho haitakuwa tofauti sana na mazingira ambayo Wekundu hao wa Msimbazi wamewahi kuyapitia huko nyuma lakini ikasonga mbele.

Ni mechi inayohitaji nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja kwa Simba kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kushinda moja ya mataji makubwa ya Afrika.

Kama itashinda taji hilo, kwa Afrika Mashariki itakuwa timu ya pili kufanya hivyo baada ya Gor Mahia ya Kenya kushinda Kombe la Washindi Afrika mwaka 1987.

Ni rekodi ambayo kila mwana Simba na Watanzania wenye mapenzi mema na mchezo wa soka wanaitamani, hivyo wasije kupoteza nafasi hii muhimu kwao kuingia kwenye vitabu vya kihistoria.

Wako nyuma kwa mabao mawili, lakini wana dakika nyingine 90 nyumbani kuwapa Watanzania raha.

Mwisho wa siku tunawatakia kila la heri Simba kwenye jukumu lao hilo nyeti la kuliheshimisha taifa kwa kunyakua
ubingwa huu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button