Kila mzigo wa taifa unahitaji bega la mzalendo (2)
WIKI iliyopita, makala hii ya RASHID JAFARI iliishia katika kipengele kinachosema kutokana na ujinga wa baadhi ya watu, wengine wanaingia katika filamu ya maigizo ya demokrasia wakivaa uhusika wa uzalendo bila kujua athari zake na malipo ya kushiriki katika filamu hizo kwamba ni kuangamiza taifa na watu wake wakiwamo
ndugu, jamaa na marafi ki zake. FUATILIA sehemu hii ya mwisho.
Malipo ya kushiriki katika filamu hizo za maigizo ya demokrasia kwa kuvaa uhusika wa uzalendo ni kupandisha watu chati, kuwapa umaarufu ambao hauna faida wala uhusiano na maendeleo ya nchi.
Mengine ni kuzorotesha maendeleo ya nchi kwa kuhamisha fikra za vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa badala ya kujikita katika shughuli za maendeleo ya nchi na wao wenyewe ambazo ndiyo msingi wa maendeleo yao na taifa. Badala yake hujikita mitandaoni kwa mijadala isiyo na tija kwa taifa.
Aidha, baada ya kutumia nguvu na muda wao vibaya kwa kubeba mabango mitaani sambamba na kuruhusu akili na nguvu zao zitumike kwa manufaa ya watu wengine, wanaharakati hao wa kisiasa na haki za binadamu, wakimaliza maigizo ya sehemu ya kwanza huhamia sehemu ya pili ambayo ndiyo kiini cha maigizo yao na ndiyo miongoni mwa malengo makuu ya maigizo hayo.
Wanamaigizo haya ya harakati huwa na malengo kadhaa ambayo ni kiini cha kufanya maigizo ili watumie
ujinga wa watu kama mtaji wa biashara yao ya maigizo na umasikini wa watu kama daraja la kuwavusha wafikie
malengo yao.
Malengo yao huwa ni kujipatia umaarufu ili wawe watu mashuhuri bila kujali athari zinazosabishwa na njia wanazotumia kupata umaarufu huo, kujipatia kipato, uungwaji mkubwa wa wananchi na taasisi za kimataifa ili kutumia uungwaji huo kama kinga kufanya maovu na kuvunja sheria kwa kivuli cha uanaharakati ili wanapoguswa na mikono ya sheria, kesi zao zisihukumiwe na mahakama kutokana na shinikizo la taasisi za kitaifa, kimataifa na pia uungwaji mkono na baadhi ya makundi ya watu.
Lengo lao kubwa ni kutafuta viza ya ukimbizi ya kwenda Ulaya au Amerika kuishi na familia zao maana huko ndiko akili na roho zao zinatamani kuishi. Hii ni kwa kuwa wanaharakati hawa wa maigizo si wazalendo wa kweli wala hawana nia njema kwa taifa na wananchi wenzao, bali wao wapo ili kujipatia sifa, umaarufu, kipato na kutafuta viza za kuishi ughabuni.
Wanaharakati hawa hawa miili yao ni ya Kiafrika maana wamezaliwa Afrika, nyama na mifupa yao imetokana na chakula kilichoota kwenye udongo wa Afrika lakini fikra na mioyo yao kwa makusudi vimeamua kusaliti nchi zao na ndugu zao na kupuuza upendo wa nchi zao.
Bila kufikiri Wazungu walitumia nguvu, jasho na damu kujenga nchi zao na kudumisha umoja na mshikamano katika nchi zao baina ya wao kwa wao na baina yao na serikali zao na kuweka misingi ya kuheshimiana na kusikilizana baina ya raia na viongozi.
Hao, wanashindwa kuchochea serikali na nchi zao kuonekana mahali salama kwa uwekezaji na ushirikiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali ambao ni wajibu wa wazalendo na misingi ya maendeleo.
Ajabu, eti jukumu lao linabaki kuwa kuwekeza akili na nguvu zao kufanya kazi kwa bidii kutengeneza taswira ya nchi zao na si kuzikimbia na kutamani kuishi kwenye nchi za wenzao ambazo wazalendo wa kweli walivuja jasho kuzitengeneza.
Wanaharakati wengi wa kizazi hiki ni waigizaji maana hawana roho za uzalendo hata chembe pia, hawana utu wa kutakia nchi zao mema. Kiukweli wao wenyewe wameshaamua nguvu na akili zao zisitumike kwa manufaa ya nchi zao, bali zitumike kwa manufaa yao binafsi na wale wanaowatumikia. Ili kufanikisha hili huwa wanaleta maigizo yenye athari mbaya kwa Waafrika.
Kwanza, wanazua taharuki na kushawishi taasisi za dunia kuwa nchi zao haziheshimu mikataba ya haki za binadamu na sheria za kimataifa. Wanajua kufanya hivyo ni njia kuu ya kujipendekeza kwa kwa kuwa wanasaidia kazi ya kuwatia hofu viongozi wa Afrika na kuwaandaa kufuata matakwa ya mabepari kirahisi.
Kutokana na kutokuwa na utu wala huruma kwa ndugu zao, ikitokea nchi inawekewa vikwazo hushangilia kwa nguvu. Hii ni ishara ya uzembe wao wa kufikiri.
Hawa, wanasababisha matatizo kwa Waafrika wenzao kutokana na midomo yao, harakati zao za masilahi binafsi ndizo zimechochea tamaa za kufanikisha malengo yao binafsi, na kutafuta hifadhi ya ukimbizi kupitia kaulimbiu ya ‘ujinga ni mtaji, umasikini wao ni daraja la kutuvusha.’
Ile hali inaondoa utu na huruma hata kwa watu wao wa karibu na kuwafanya wapate tabu ikiwemo ndugu zao ukoo mmoja, kabila lake, watu wa dini na madhehebu yao, watu wa kijiji, wilaya, mkoa na nchi yake. Kwa tafsiri fupi, watu hawa huwa na laana inayosababishwa na malezi mabaya ya kukosa utu, uungwana na upendo kwa watu wako na kukosa imani chanya juu ya taifa.
Ndiyo maana hawaoni tabu kuwatoa kafara ndugu zao, watu wao wa karibu na hatima ya nchi yao. Wanafanya hivyo kupata sifa za kijinga, masilahi binafsi na kusukumwa na tamaa ya kutafuta hifadhi za ukimbizi nchi za ng’ambo.
Uzalendo wa kweli ni utayari wa kubeba sehemu ya mzigo wa taifa Mzigo wa taifa ni changamoto, majukumu na gharama zinazohusiana na uendeshaji wa nchi na ustawi wa wananchi wake. Mzigo huu unaweza kuainishwa kama mzigo wa kiuchumi.
Kusaidia kubeba sehemu ya mzigo wa taifa kwa kusaidia nchi kupata uwezo wa kugharamia huduma za msingi kama afya, elimu, miundombinu, vyanzo vya nishati na usalama, kulipa madeni ya taifa, kupambana na umasikini, ukosefu wa ajira kuongeza mapato ya nchi kupitia kulipa Kodi.
Mzigo wa kijamii
Wananchi wanatakiwa kusaidia kubeba sehemu ya mzigo wa taifa wa kijamii kwa kuhakikisha usawa, mshikamano na haki miongoni mwa raia, kupambana na rushwa, ujinga na maovu ya kijamii, kuhifadhi maadili na utamaduni na amani ya nchi.
Mzigo wa kisiasa
Wananchi wanatakiwa kusaidia kubeba sehemu ya mzigo wa taifa kisiasa na kiutawala, kwa kuweka shinikizo kwa viongozi wawajibike katika majukumu yao, kushiriki katika michakato ya kidemokrasia kama kupiga kura, kujitokeza kutoa maoni ya kuchangia ustawi wa taifa kwa heshima na kwa kutumia lugha ya kujenga taifa si ya kuleta mipasuko na migawanyiko katika jamii pamoja na kutii sheria na kutoa ushirikiano chanya kwa taasisi za umma.
Kutekeleza jukumu la raia la kubeba mzigo wa taifa Hii inamaanisha raia kushiriki kikamilifu kutatua changamoto hizi, kupitia matendo ya kila siku yanayosaidia kujenga nchi.
Raia wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo nchini Ili kujiingizia kipato na kuinua uchumi wa kaya zao na taifa kwa kulipa kodi na ushuru kupitia shughuli zao za kila siku za uzalishaji na kujitafutia ridhiki.
Kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ni jukumu mama la raia na ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya nchi na pia, ndiyo njia kuu ya kubeba sehemu ya mzigo wa taifa na kuleta ustawi wa nchi na wananchi.
Maisha ya kila siku ni uwanja wa maandamano ya uzalendo wa moyoni, unapolima unatetea nchi kwa kuchangia ustawi wake, unawezesha upatikanaji wa malighafi na viwanda kufanya kazi ili kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, na kuwa pia unazalisha chakula kusaidia kuleta utulivu katika nchi na usalama kuzuia majanga ya njaa.
Aidha, unalipa ushuru au kodi kwa nchi, wewe mkulima na wenzako mnaojishughulisha na uzalishaji wa uchumi kupitia sekta binafsi au za umma, ninyi ndio wazalendo wa kweli na mnayoitakia nchi mema, nguvu na akili zenu mnazitumia vizuri kwa manufaa ya nchi.
Pia, bila kuwasahau watumishi wa umma na sekta binafsi mnaofanya kazi na shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa kwenye mazingira mbalimbali magumu na mepesi na kuhakisha mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo, nyinyi ndio wazalendo wa kweli, mnatetea hadhi ya nchi kwa vitendo na kutengeneza mustakabali bora wa nchi na wananchi.
Shughuli za kila siku ni mapambano halisi juu ya uzalendo wa moyoni usiohitaji kushangiliwa, wala mitandao ya kijamii na mikutano kujulikana. Huu ndiyo uzalendo wa kweli unaotatua changamoto za kijamii, uchumi na kisiasa na ndiyo ishara ya utayari wa kubeba sehemu ya mzigo wa taifa, kutetea nchi na kuweka msingi wa maendeleo ya nchi.
Mfano madaktari kila siku kazini wanapambana na maradhi kuhakikisha afya za watu zinakuwa bora, ili waweze kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa bidii. Wakulima wanapambana mashambani kuhakikisha nchi ina chakula cha kutosha, na pia viwanda vinapata malighafi na sekta ya viwanda inakua.
Walimu wanapambanana shuleni, vyuoni kila siku ujinga na kuhakikisha watu wana maarifa ya kutosha ya kuweza kutumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuhakikisha nchi inasonga mbele. Wafanyabiara, mamalishe, wamachinga pia wanapambana kila kukicha kuhakikisha wanainua uchumi wa kaya zao na nchi kwa ujumla.



