Kila watu 8, mmoja ana tatizo afya ya akili

MTU mmoja katika kila watu nane imeelezwa kuwa hivi sasa ana tatizo la ugonjwa wa afya ya akili, wakati awali ilikuwa mtu mmoja katika kila watu 10.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), katika mwongo  mmoja uliopita, kumekuwa na ongezeko la watu kwa asilimia 13, ambapo watu bilioni 1 wanaishi na tatizo hilo duniani.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Wiki ya Afya ya Akili, Mwakilishi wa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI), ambaye ni  Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema Madenge  amesema Tanzania inakadiriwa kuwa wa wagonjwa milioni 7 wenye matatizo hayo na wengi wao wanaishi na sonona.

“Sambamba na ongezeko la ugonjwa wa akili, lakini pia kumekuwa na matukio ya kikatili ambapo wanawake wanne kati ya 10 wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 45 wamefanyiwa ukatili wa kimwili.

“Pia  wanawake wawili kati ya 10 wamefanyiwa ukatili wa kingono  na hao wote baada ya kufanyiwa ukatili huu wanaelekea kwenye tatizo la afya ya akili,” amesema.

Madenge ameeleza kuwa sababu kubwa ya magonjwa ya akili na ukatili ni mabadiliko katika mfumo wa malezi ya familia, msongo wa mawazo wa kushindwa kuhimili changamoto, ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na matumizi ya vilevi hususan pombe, bangi na dawa zingine za kulevya.

Habari Zifananazo

Back to top button