Kilele cha Mkutano wa FOCAC na mustakabali wa Afrika
MKUTANO wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) mwaka 2024 utafanyika Beijing, China kuanzia Septemba 4 hadi 6.
Katika mkutano huo pamoja na mambo mengine tangu kuanza kwake, nchi za Afrika zimeonekana kunufaika zaidi na ushirikiano huo kutoka China.
Mkutano wa Focac hufanyika kila baada ya miaka mitatu na katika miaka ya karibuni, umekuwa miongoni mwa mikutano muhimu Katika uhusiano wa kimkakati baina ya nchi za Afrika na China.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Hua Chunying anasema mkutano huo una kaulimbiu isemayo: ‘Kushikamana Kuhimiza Ujenzi wa Mambo ya Kisasa na Kujenga Jumuiya ya Kiwango cha Juu ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja.’
Mkutano huo utawakutanisha viongozi na wakuu wa nchi za Afrika, wawakilishi wa mashirika husika ya kikanda ya Afrika, mashirika ya kimataifa na wadau wengine walioalikwa.
Mkutano huo ni wa nne kufanywa na jukwaa hilo na utazungumzia masuala ya urafiki, ushirikiano na mustakabali wa uhusiano wao wa baadaye.
Mchambuzi na Masuala ya Uchumi na Siasa, ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi anasema Focac, China imeleta manufaa mengi zaidi kwa nchi za Afrika kuliko nchi za Magharibi.
Profesa Moshi anasema China imekuwa mshirika na mdau muhimu kusaidia sekta mbalimbali barani Afrika kama vile biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege.
Aidha, mchango wao umeonekana pia katika miradi ya uzalishaji umeme, mambo yanayochangia maendeleo ya Afrika.
Katika mkutano kama huo wa Focac uliofanyika mwaka 2021 mjini Dakar nchini Senegal, Profesa Moshi alishauri ulenge kuimarisha miundombinu ya afya katika Afrika ili baadaye iweze kukabiliana na majanga kama janga la Covid -19.
Aidha, alishauri kuangaliwa namna ya kuimarisha teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na kuondoa pengo lililopo kati ya miji na vijiji katika ufikiwaji wa tknolojia hiyo.
Katika ufunguzi wa mkutano uliopita, mwito ulitolewa wa kuimarisha zaidi ushirikiano utakaoleta faida sawa kwa pande zote mbili.
Mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na masuala ya biashara na usalama. Viongozi na wakuu wa nchi walishauri kuongezeka kwa ushirikiano katika maeneo hayo ili kuwa na tija zaidi kupitia ushirika wao.
Inatarajiwa kuwa, mkutano wa mwaka huu utatanguliwa na mikutano ya maofisa wa ngazi za juu na mawaziri itakayofanyika Septemba 2 na 3 kufanya maandalizi ya mkutano huo wa kilele.
Septemba 4 hadi 6, shughuli mbalimbali mfululizo zitafanyika ikiwa ni pamoja na hafla ya ufunguzi wa mkutano, halfa ya mchapalo, maonesho ya michezo ya sanaa, mikutano sambamba ya ngazi ya juu, mkutano wa wajasiriamali wa China na Afrika na mikutano ya pande mbilimbili.
Profesa Song Wei wa Shule ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia katika Chuo Kikuu cha Kigeni cha Beijing anabainisha kuwa, baada ya Covid-19, nchi za Afrika kama zilivyo nchi nyingine zinakabiliwa na changamoto kadha wa kadha.
Hivyo kupitia mkutano huo, masuala ya ushirikiano kati ya China na Afrika yanatarajiwa kuongezeka zaidi na huenda ukajumuisha masuala ya ufadhili wa kifedha, ushirikiano katika mageuzi ya viwanda ili kufanya Bara la Afrika kuwa la kisasa zaidi.
Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amethibitisha kupokea mwaliko rasmi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kushiriki mkutano huo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping.
Mwaliko huo umewasilishwa na Balozi wa China nchini, Chen Mingjian. Umebainisha nafasi ya kipekee kwa Rais Samia kuzungumza katika kikao cha ufunguzi kwa niaba ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais Samia kwa mujibu wa mwaliko huo, anatarajiwa kuzungumza katika mkutano wa ngazi ya juu utakaojadili mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa.
Kombo anasema nafasi ya Rais Samia kushiriki na kuzungumza katika jukwaa hilo itaipa nchi fursa ya kuangazia uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Hatua hii itasaidia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo Tanzania ni kinara na kiongozi wa kuigwa kwenye jumuiya hiyo kongwe Afrika,” anasema.
Balozi Kombo amesema Tanzania itashiriki mkutano huo utakaotoa tamko la Focac na mpango kazi wake utakuwa moja ya matokeo ya mkutano huo.
Balozi Chen yeye anasema China imefurahishwa na kupokewa kwa mwaliko huo na kwamba, hatua hiyo itakuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na China.
“China inaiona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na tunaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania,’’ anasema Chen.
China na Tanzania zimekuwa na uhusiano na urafiki uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 na hivi karibuni taifa hilo lilitangaza kuendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania katika zama mpya za uhusiano wa kidiplomasia wenye lengo la kujenga dunia iliyo bora yenye maendeleo na usalama zaidi.
Baadhi ya maeneo ambayo China imekubali kushirikiana na Tanzania ni uboreshaji wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim ikiwemo kuongeza majengo, mitaala na kukifanya cha kutengeneza ajenda kwa ajili ya masuala ya kimkakati ya kubadili mfumo wa uendeshaji wa dunia.
Dk Salim ni mmoja wa wanadiplomasia wa Tanzania anayeheshimika na kuridhiwa kwa ombi hilo la Tanzania kwa China kuongeza hadhi ya chuo hicho na hadhi ya kidiplomasia na umuhimu wake kwa nchi hizo mbili.
Mbali na hayo, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la uwekezaji kutoka China katika miradi mbalimbali nchini ambayo kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), kuanzia Januari 2021 hadi Desemba 2023 jumla ya miradi 256 ya China imesajiliwa nchini yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 2.4
Aidha, miradi hiyo imetengeneza fursa za ajira 29,122 na miradi hiyo ni ya uwekezaji katika uzalishaji, kilimo, huduma na nyinginezo.
Jukwaa la Focac lilianzishwa kukuza ushirikiano kati ya China na Afrika ili kuchagiza maendeleo kupitia sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Limekuwa jukwaa linalotoa fursa sawa kwa pande zote mbili kujadili masuala muhimu ya kimaendeleo na kutafuta majawabu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo amani na usalama na mabadiliko ya tabianchi.