Mabilioni biashara ya kaboni hatarini kutoweka

KATAVI; Licha ya vijiji vinane vya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kujiingizia zaidi ya Sh bilioni 29 kupitia uuzaji wa kaboni, biashara hiyo ipo hatarini kutokana na uwajibikaji usioridhisha wa waliopewa dhamana ya kulinda na kuhifadhi misitu na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu.
Uchunguzi wa miezi mitatu uliofanywa katika Vijiji vya Katuma, Bujombe, Kafisha, Kaseganyama, Songambele, Nkungwi, Ikola na Karema mkoani Katavi umebaini kuwa kumekuwa na mchuano mkubwa kati ya wahifadhi wa misitu na wananchi.
Katika uchunguzi huo, imebainika pasi na shaka kwamba licha ya mafanikio makubwa ya kifedha yanayopatikana kutokana na biashara hiyo yenye lengo la kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi (hasa hewa ya ukaa – carbon dioxide) kwa kuweka thamani ya kifedha kwenye utoaji wa hewa hiyo, ili kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na uwekezaji katika miradi rafiki kwa tabianchi, kinachoendelea kwenye usimamizi wa misitu kinaashiria hatari kubwa ya kimazingira na kifedha sawia.
Misitu inapungua, mashamba yanaongezeka
Katika baadhi ya vijiji vilivyotembelewa, mipaka ya misitu ya kijiji inaonekana kusogezwa taratibu na mashamba mapya ya mahindi, maharagwe na mpunga yanaongezeka. Wananchi wanasema ongezeko la watu na kupungua kwa rutuba ya ardhi ya miombo kunawalazimisha kutafuta maeneo mapya ya kulima.
Mkazi wa Kijiji cha Katuma, Rehema Hassan anasema: “zamani maji yalikuwa karibu. Sasa tunatembea zaidi ya kilomita moja wakati wa kiangazi. Hata kuni zilikuwa karibu, leo tunazifuata mbali.”
Kauli yake inaakisi mabadiliko yanayohisiwa moja kwa moja na jamii. Kwa mujibu wa takwimu za sensa, idadi ya watu katika Wilaya ya Tanganyika imeongezeka kati ya mwaka 2012 na 2022, hali inayoongeza shinikizo la ardhi kwa ajili ya makazi na kilimo.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2012 Tanganyika ilikuwa na jumla ya wakazi 179,136 ikilinganishwa na watu 371,836 katika sensa ya mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la watu 192,700. ambao ni sawa na asilimia 51.
Ongezeko hilo linamaanisha kwamba idadi hiyo ya wakazi inahitaji kujenga nyumba za makazi, biashara, huduma za kijamii na nyinginezo huku wengi wao wakihitaji maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo sambamba na mifugo na hivyo kumega sehemu ya misitu kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo.
Wilaya ya Tanganyika ina zaidi ya hekta milioni moja za misitu ya hifadhi, ikiwemo misitu ya vijiji na misitu ya halmashauri inayolindwa chini ya miradi mbalimbali ya uhifadhi kama miradi ya biashara ya Kaboni, hata hivyo juhudi za kuzipata takwimu halisi za kuoesha kuwa miaka 10 iliyopita eneo la msitu katika wilaya hiyo lilikuwa na ukubwa kiasi gani na mpaka sasa limeporomoka hadi kufikia kiasi gani hazikuzaa matunda licha ya chanzo hiki kufuatilia kwa kina.
Miaka ya hivi karibuni Tanzania inapoteza misitu kwa kasi kutokana na shughuli za binadamu. Kwa mujibu wa National Environmental Statistics Report (NESR,2017) Tanzania inapoteza hekta 372,000 za misitu kila mwaka kutokana na ukataji wa miti, kilimo na makazi ya watu.
Hata hivyo data za ufuatiliaji wa misitu misitu kwa kutumia satellite (kama Global Forest Watch) zinaonesha kuwa Mkoa wa Katavi ulipoteza takribani hekta 17,035 za misitu mwaka 2023 pekee kutokana ukataji miti,kilimo na shughuli nyingine za binadamu.
Sheria zipo nani anayewajibika?
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, vijiji vina mamlaka ya kusimamia misitu yao kupitia Kamati za Maliasili. Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Tanganyika, Joseph Bisura anakiri kuwapo kwa changamoto, “rasilimali za kufanya doria ni ndogo. Pia bado kuna wananchi hawajaelewa kikamilifu umuhimu wa kulinda misitu.”
Hata hivyo, kauli yake inapingwa na baadhi ya wakazi hao ambao kwao, tatizo si uelewa pekee. Mkulima mmoja wa Bujombe ambaye aliomba kutotajwa jina, anasema, “kama sheria zipo, kwa nini watu wanaendelea kukata miti waziwazi? Wakati mwingine tunaona kama hakuna anayewajibika.”
Kuhusu hoja ya kuwajibika, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika, Hamad Mapengo, anasema: “Tumepitisha maazimio ya kulinda mazingira. Changamoto ipo kwenye utekelezaji ngazi za chini. Uwajibikaji lazima uimarishwe.”
Kauli ya mwenyekiti inaonesha kuwapo kwa pengo kubwa kati ya maandishi ya kisheria na uhalisia wa utekelezaji vijijini.
Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Tanganyika, Bruno Mwaisaka amesema mara kadhaa wamechukua hatua ya kutoa elimu kwa kwa viongozi wa ngazi ya vijiji ili kuhakikisha wanakumbushwa wajibu wao katika jukumu zima la utunzaji wa misitu.
Kwa wale wanaopindisha sheria hizo za utunzaji wa mazingira Mwaisaka ametolea mfano wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kagunga Tunka Kuwasanya ambaye alihukukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya shilingi laki tano kwa kosa la kutosimamia vyema sheria hizo.
Hata hivyo kwa Halmashauri hiyo bajeti inayopaswa kutolewa kwa ajili ya usimamizi wa misitu ni shilingi bilioni 1.1 kwa mwaka huku bajeti halisi inayotolewa ni shilingi milioni 300 hali inayosababisha idara ya maliasili kukwama kutelekeza shughuli zake kwa ufasaha.

Mwaisaka anasema anaamini kiasi hicho cha shilingi bilioni 1.1 kingetolewa changamoto nyingi za utunzaji wa misitu zingetatuliwa na tatizo hilo kupungua kwa asilimia zaidi ya 80.
Hata hivyo wamechukua hatua ya kutoa elimu kwa viongozi na wananchi ambapo elimu hiyo hutolewa mara 4 kwa mwaka kwa maana ya kila baada ya miezi mitatu huku ikitajwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa wilaya hiyo wamefikiwa na elimu. Kadhalika, hakuna tathmini yoyote iliyofanyika baada ya limu hiyo.
Biashara ya kaboni: Fursa kubwa, hatari kubwa
Kupitia ushirikiano na kampuni ya Carbon Tanzania, vijiji vinanufaika mara mbili; kwanza kifedha kutokana na kuuza kaboni lakini jambo jingine ni kulinda misitu yao.
Fedha zinazotokana na biashara hiyo zimeelekezwa kwenye miradi ya shule, zahanati na miundombinu ya kijamii.
Kutokana na fedha za Mradi wa Kaboni Zahanati 7 zilijengwa zenye uwezo wa kupokea wagonjwa wa nje na wa ndani ambapo kabla ya uwepo wa Zahanati hizo wakazi wa vijiji hivyo walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Mwaisaka anabainisha kuwa “Tulifanya ujenzi wa kituo cha afya Katuma kwa kujenga majengo ya mama na mtoto, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia na jengo la wagonjwa wa nje OPD.
“Ununuzi wa vifaa tiba na dawa kwa zahanati za vijiji vya katuma, kapanga, lwega, mpembe, kagunga, lugonesi na bujombe vyenye thamani ya Tsh 700,000,000. Ujenzi wa zahanati ya kitongoji cha Manyonyi. Ujezi wa zahanati wa vijiji 7. Ukamilishaji wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) kata ya mwese.
“Ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya two in one katika vijiji vya Kapanga, Lwega, Kagunga, Mpembe na three in one Lugonesi. Ujenzi wa matundu ya vyoo 46 kwa zahanati za lwega, bujombe, Mpembe, Kapanga, Lugonesi na manyonyi. Ujenzi wa vichomea taka vya kisasa kwa zahanati za lugonesi, katuma, lwega, kapanga, mpembe, mwese na kituo cha afya Katuma.”
“Katika Sekta ya Kilimo mradi huo metekeleza ujenzi wa majosho 03 kwa vijiji vya Kapanga, Lwega na Bujombe. Huku Sekta ya Elimu kukiwa na ujenzi wa vyumba 27 vya madarasa katika vijiji nane vya mradi wa Kaboni, ukarabati wa vyumba 19 vya madarasa katika vijiji nane, ujenzi wa nyumba 09 za walimu (two in one) na nyumba mbili (single) katika shule za msingi za vijiji.
“Ujenzi wa matundu 24 ya vyoo katika shule za msingi za vijiji vinavyonufaika na biashara ya Carboni. Ujenzi wa jiko na stoo na utoaji wa chakula wa wanafunzi katika Shule za msingi 17.
“Kwa upande wa Elimu ya Sekondari umefanyika ukarabati wa vyumba 07 vya madarasa shule ya sekondari Mwese, Ujenzi wa Sekondari ya Bujombe, Ujenzi wa vyumba 04 vya madarasa na vyoo matundu 08 sekondari ya bujombe, Ujenzi wa bwalo la chakula pamoja na jiko katika sekondari ya Mwese, Ujenzi wa mabweni 02 ya wavulana na wasichana sekondari ya Mwese, ununuzi wa vitanda na magodoro 240 katika shule ya sekondari ya Mwese na Utoaji wa chakula kwenye Secondari za Mwese na Kagunga,” anasema.
Sekta ya Utawala ujenzi wa nyumba 08 za watendaji wa vijiji vyote vya Biashara ya Kaboni, Ujenzi wa ofisi 08 za vijiji vya biashara ya Carbon, Ujenzi wa ofisi 01 ya kata ya kasekese, Ununuzi wa pikipiki 20 kwa ajili ya shughuli za doria na utawala, Uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi kupitia COCOBA kwa vikundi 47 vya kijamii katika vijiji vya biashara ya carboni.
Sekta ya Maliasili, Uwekezaji bikoni na upakaji wa rangi miti kwenye mipaka ya misitu ya vijiji vyote nane vya Kaboni, Ununuzi wa magari wawili land cruiser kwa ajili ya Doria, ajira kwa wananchi 112 kwenye kamati za maliasili za vijiji.
Sekta ya Viwanda na Biashara, ujenzi wa masoko 03 ya vijiji vya katuma, Mwese na Lugonesi na ujenzi wa vyumba 10 vya maduka katika kijiji cha Katuma. Huku Sekta ya Miundombinu ujenzi wa daraja/karavati na uwekaji wa kifusi katika barabara ya kijiji cha Lugonesi.
Faida za ujumla biashara ya kaboni
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imenufaika moja kwa moja pamoja na vijiji vyake 8 kwa mapato yanayotokana na biashara ya Kaboni inayoendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika halmashauri.
Wilaya ya Tanganyika imeweza kufahamika nchi nzima kutokana na Biashara ya Kaboni na halmashauri nyingi zinazidi kuja Tanganyika kujifunza biashara ya kaboni, hadi sasa zaidi ya halmashauri 80 zimeshapokelewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imekuwa ni mfano kwa nchi nzima juu ya Biashara ya Kaboni na viongozi wa kitaifa wamekuwa wakizielekeza Halmashauri mbalimbali kuja Tanganyika kujifunza fursa mpya ya Biashara ya Kabon.
Kwa ujumla mzunguko wa fedha uliotokana na biashara ya Kaboni umechangia kuongeza ajira kwa wananchi na kuwanyanyua kiuchumi.
Thamani ya Misitu katika Halmashauri ya Tanganyika imeendelea kupanda kutokana na Biashara ya Kaboni.
Hatari kubwa
Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Tanganyika, Bruno Mwaisaka, anasema, “mvua zisizotabirika na mavuno hafifu vinawasukuma wakulima kupanua mashamba. Bila kuongeza tija ya kilimo, tutakuwa tunazunguka tatizo.”
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Katuma, Yassin Kapaya, anatahadharisha, “Tukiharibu misitu, wawekezaji wataondoka. Hizo bilioni hazitarudi tena.”

Hapa ndipo mgongano ulipo; wananchi wanahitaji ardhi kuishi leo, lakini mapato ya kaboni yanategemea misitu ibaki kesho.




JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 12000-16700 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..
.
This is my main concern…………………… http://Www.Cash54.Com
I just came across this amazing way to earn $11,000-$15,000 a month online! No selling, no struggle—just a simple system that anyone can follow. Mia Westbrook did it, and so can you! Don’t miss out on this life-changing opportunity.
.
This is what I do…………………… http://Www.Payathome9.Com