HALMASHAURI ya Mji wa Geita imejiwekea utaratibu wa kujenga takribani kilomita nne za lami kila mwaka ili kuongeza mtandao wa barabara za lami.
Utaratibu huo unahusisha kilomita zisizopungua mbili za barabara kwa mapato ya ndani kila mwaka na kilomita zingine mbili kupitia pesa za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR).
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu amesema hayo mbele ya wananchi na viongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2024 walipofika kuizindua barabara ya Q man- Lukirini mjini Geita.
Amesema halmashauri inashirikiana na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) kujenga barabara za lami kwa kuanza na barabara za kata ya Kalangalala ambayo ndio kitovu cha mji wa Geita.
“Nafahamu zipo barabara nyingi mbovu na zingine zina hali mbaya sana, wapo wakandarasi ambao wameshapatikana kupitia Tarura wanaendelea kutengeneza.
“Kwa barabara zile ambazo hazijatengenezwa mwaka wa fedha ulioisha tayari tumeshakaa kuona ni barabara gani tunaweza kuzitengeneza,” amesema Kanyasu.
Amesema kwenye jimbo la Geita mjini ujenzi wa takribani Km 17 za barabara za lami unaendelea na ujenzi wa Km 17 ikiwemo kilomita moja inayojengwa kwa ufadhili wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kanyasu amesema kukamilika Km 17 pamoja na kilomita nne za lami kila mwaka mji wa Geita utafikia asilimia 15 ya mtandao wa lami
Mhandisi wa Halmashauri, Mhandisi Makongoro Igungu amesema Ujenzi wa Lami nyepesi ya Q Man – Lukirini ya Km 1.28 umetekelezwa na mkandarasi EVANCE CONSTRUCTION Ltd kwa Sh milioni 851.3 mapato ya ndani.
Amesema mradi umesimamiwa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Geita kwa utekelezaji wa miezi 11 kuanzia Juni 2024.
“Hadi sasa mradi umegharimu Sh milioni 835.3 na mpaka sasa umefikia asilimia 100 ya utekelezaji ambapo kazi zilizofanyika ni kuchimba na kusafisha njia.
“Manufaa ya mradi ni kurahisisha usafirishaji kwa kipindi chote cha mwaka, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuongeza thamani na kupendezesha manzari ya mji na kupunguza msongamano,” amesema Igungu.