Kinana awapa CCM mbinu ya ushindi

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, amewataka viongozi wa chama hicho kuwa wamoja kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Kinana amesema hayo leo Julai 23, 2023, wakati akizungumza na viongozi wa CCM katika kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.

“Napongeza kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa CCM hususan kuanzia kitongoji, kijiji, mtaa na Kata kwa kazi nzuri mnayoifanya,” amesema na kuongeza:

“Mwakani ni mwaka wa uchaguzi, hivyo naamini wana CCM tutakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwaka 2024 tukiwa kitu kimoja, tukifanya kampeni wamoja na tutaibuka na ushindi tukiwa wamoja, hivyo hivyo katika uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema Kinana.

Kinana, amesema chama  kinatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na viongozi wa CCM katika ngazi za kata, vitongoji, vijiji, wilaya na mkoa kwani wao ndio wanaokutana na wananchi na wakati wa uchaguzi ndio wanaoenda kuomba kura.

Pia amewapongeza madiwani wanaotokana na CCM, ambao wamekuwa wakisimamia ngazi ya kata na wamekuwa wakifanya hivyo bila ya kuwa na mshahara.

Kinana ameanza ziara leo Julai 23,2023 katika mikoa mitano  ya kukagua utekekezaji wa ilani ya CCM, ziara ambayo itafikia tamati Agosti Mosi. 

 

Habari Zifananazo

Back to top button