Kinondoni yanufaika ujenzi wa barabara
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius Ndejembi amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 Jimbo la Kinondoni ilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 4.87 kwa ajili ya kazi za Ujenzi na Matengenezo ya barabara zenye jumla ya kilomita 26.52.
Ameeleza hayo wakati alijibu Swali la Tarimba Abbas,Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, aliyetaka kujua Je, ni lini Serikali itawaongezea TARURA bajeti ili barabara za ndani za Jimbo la Kinondoni
zijengwe kwa kiwango cha lami.
Ndejembi amesema matengenezo ya kawaida ni kilomita 24.32 na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa 2.2 ambapo utekelezaji wake unaendelea na umefikia asilimia 70 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 29 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22.
Aidha, amesema Serikali imekuwa ikiongeza bajeti kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara ambapo katika mwaka wa fedha 2021/22, Jimbo la Kinondoni lilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 2.38 ambazo zilitekeleza matengenezo ya barabara ya jumla kilomita 26za lami na changarawe na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 0.52.
Ndejembi amesema jimbo la Kinondoni lina mtandao wa barabara wenye urefu wa jumla ya kilomita 231.571.Kati ya hizo kilomita 69.867ni barabara zenye tabaka la lami na zege,kilometa 137.833 ni barabara zenye tabaka la Changarawe na kilomita 23.871 ni barabara za zenye tabaka la udongo.