Kisa cha baba aliyenyanyaswa kwenye ndoa miaka 25

Katika kijiji cha Isakalilo, kata ya Kalenga, wilayani Iringa, Patrick Ngasapa, mwenye umri wa miaka 59, anasimulia changamoto ya ndoa yake ya miaka 25, ambayo imegubikwa na migogoro ya mara kwa mara.

Hali hii imemfanya kukata tamaa huku akikosa msaada wa kutosha kurekebisha hali ya familia yake.

Kisa chake ni mfano halisi wa tatizo la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume, ambalo mara nyingi hupuuziwa na jamii.

Advertisement

HISTORIA YA TATIZO

Ngasapa anasema matatizo katika ndoa yake yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya mke wake (hakutaka kumtaja jina) kushirikisha familia yake ya asili katika mambo ya ndoa.

“Chochote kinachotokea nyumbani kwetu, lazima kiwafikie mama, baba, kaka, na dada zake. Na jambo likifika huko linakuzwa, na hatimaye mke wangu huondoka nyumbani na kwenda kwao,” anasema.

Mara ya mwisho, Februari, 2024, anasema mke wake alihama nyumbani akiwa na watoto wao watatu, ambao wako katika madarasa tofauti – mmoja akiwa sekondari, na wawili wakiwa shule ya msingi.

“Kilichochochea hatua hiyo ni mzozo mdogo kati ya mama na mtoto wetu, jambo ambalo lilitafsiriwa vibaya kwamba ninamlisha mtoto maneno ya kumjibu mama yake. Sasa yuko kwa wazazi wake, na amesema ameomba talaka, ingawa mchakato huo haujakamilika,” anaeleza.

MZIGO WA MALEZI NA CHANGAMOTO ZA KISHERIA

Tangu mke wake aondoke, Ngasapa amekuwa akilazimika kuhudumia watoto wakiwa nyumbani kwa bibi yao, huku Ustawi wa Jamii ukimpa majukumu mazito.

“Nimepangiwa kupeleka debe moja la mahindi, kilo tatu za maharage, na Sh 30,000 kwa kila mtoto kwa ajili ya nauli za kwenda shule kila mwezi. Mimi ni mkulima mdogo, uwezo wangu ni mdogo sana kugawanya nachopata kulea familia,” anasema kwa huzuni.

Licha ya juhudi za kuwasiliana na mke wake ili warejee pamoja na kusuluhisha matatizo yao, Ngasapa anakiri kuwa mpango huo haujazaa matunda.

“Ningependa tupate nafasi ya kusameheana kama kuna makosa tumefanya na kuanza upya kama familia kwasababu pia sifikirii kuoa mwanamke mwingine labda talaka itolewe rasmi,” anasisitiza.

UKUBWA WA TATIZO LA UKATILI

Ingawa visa vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake vinapata umaarufu zaidi, wanaume pia wanakabiliwa na aina hii ya ukatili.

Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni, pamoja na kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi za idadi kubwa ya wanaume kufanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao, wanaume wachache sana huripoti unyanyasaji wanaofanyiwa.

“Mwaka jana, tulipokea ripoti za wanaume sita pekee waliodai kufanyiwa ukatili. Hata hivyo, kuna idadi kubwa ya wanaume wanaokumbwa na changamoto hizi lakini hawajitokezi kwa hofu ya kunyanyapaliwa,” anasema.

Anasema zaidi ya asilimia 90 ya wanawake mkoani Iringa wamepata elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, na wengi wao sasa wanajitokeza kuripoti matukio hayo bila woga wowote.

Hali hiyo anasema ni tofauti kwa wanaume, ambao mara nyingi huona aibu au hofu ya kudhalilika wakiripoti unyanyasaji wa aina yoyote.

SABABU ZA UKATILI KWA WANAUME

Mgeni anasema sababu kuu za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume ni pamoja na:

Mfumo dume: Ingawa mfumo dume mara nyingi unaathiri wanawake, pia huwazuia wanaume kuonyesha hisia zao au kujitetea wanaponyanyaswa.

Uchumi duni: Kukosa uwezo wa kifedha kunafanya baadhi ya wanaume kushindwa kukidhi mahitaji ya familia, jambo linalochochea migogoro.

Mwanaume kusahaulika: Kampeni nyingi za kijinsia zimejikita kwa wanawake na watoto, huku mahitaji ya wanaume yakipuuzwa.

Utamaduni: Jamii nyingi bado zinawaona wanaume kama “walinzi wa familia,” na kuwahukumu wanaposhindwa kukabiliana na changamoto za nyumbani.

TAKWIMU ZA KITAIFA NA KIMATAIFA

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2022 inaonyesha kuwa karibu asilimia 10 ya wanaume duniani wanakumbwa na aina fulani ya ukatili wa kijinsia katika maisha yao.

Nchini, ripoti ya Tathmini ya Hali ya Usawa wa Kijinsia ya 2021 inaonyesha kuwa asilimia 6 ya wanaume wamekumbana na ukatili wa kijinsia, lakini wengi wao hawaripoti matukio hayo.

Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani ya Januari na Desemba, 2023 iliyotolewa Julai mwaka huu na Jeshi la Polisi Tanzania na kuchapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha waathirika 22,147 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima waliripotiwa na kati yao wanawake walikuwa 13,322 na wanaume 8,825.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa aina kuu za ukatili zilizoripotiwa ni pamoja na ubakaji, vipigo, ukatili wa kisaikolojia, na mauaji.

Akizungumzia namna ya kushughulikia ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume, Mgeni anataja mambo makubwa manne yanayoweza kuwa tiba ya changamoto hiyo:

Elimu ya jinsia kwa pande zote: Mashirika ya kijamii yanapaswa kuanzisha kampeni za kuwafikia wanaume ili kuwapa nafasi ya kueleza changamoto zao.

Ushauri nasaha: Kuanzisha vituo vya ushauri kwa wanaume walioathirika na migogoro ya kifamilia.

Kuimarisha dawati la jinsia: Kuweka dawati la jinsia linalowajumuisha wanaume na wanawake kwa usawa.

Ushirikiano wa viongozi wa kijamii: Viongozi wa kijiji na kata wanapaswa kushiriki kikamilifu kusaidia familia zenye migogoro badala ya kuwa watazamaji.

TGNP YATOA MAFUNZO

Kwa bahati nzuri, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umekuwa ukifanya juhudi kubwa kupambana na ukatili wa kijinsia wilayani Iringa, ikiwa ni pamoja na kata ya Isakalilo.

Mafunzo ya siku tano yaliyotolewa na TGNP katika kata ya Kalenga yamesaidia kukuza uelewa juu ya mbinu za kutokomeza ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wanaume katika majadiliano ya usawa wa kijinsia.

Mary Msemwa, mwezeshaji wa mafunzo hayo, anasema sababu za kitamaduni na kijamii, uchumi, kisaikolojia, kisheria, na vita na mizozo ya kisiasa (kwa maeneo yenye changanoto hiyo) zimekuwa vyanzo vikuu vya ukatili wa kijinsia.

Anasema mafunzo hayo yamewasaidia washiriki kutambua jukumu lao katika kuleta mabadiliko, na mpango kazi ulioandaliwa na washiriki wa mafunzo hayo unalenga kupunguza visa vya ukatili kwa kuhimiza majadiliano na elimu ya kijinsia katika familia na jamii kwa ujumla.

Mshiriki kutoka kijiji cha Isakalilo, Peter Mvula, alieleza jinsi mafunzo hayo yalivyomfumbua macho kuhusu athari za mfumo dume katika jamii na kuahidi kuwa balozi wa kuelimisha wanaume wenzake.

“Tumegundua kuwa ukatili hauna jinsia; wanaume pia wanakabiliwa, lakini wanakosa ujasiri wa kusema,” anasema Mvula.

Diwani wa kata ya Kalenga, Shakira Kiwanga, aliwataka washiriki kuwa mabalozi wa mabadiliko.

“Kupitia mafunzo haya, tunaweza kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia na kupunguza unyanyasaji kwa jinsia zote,” alisema Kiwanga.