Kiswaga aanza safari ya pili kuingia bungeni

Mbio za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 zimeanza kuchukua njia yake katika Jimbo la Kalenga, baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Jackson Kiswaga, kuchukua rasmi fomu ya uteuzi katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kuwania tena nafasi hiyo.
Kiswaga, ambaye hivi karibuni alipitishwa na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa ubunge kwa mara nyingine katika jimbo hilo, anakwenda kukabiliana na mpinzani wake Godlove Lwelu wa chama cha Chaumma.

Fomu hiyo ya uteuzi alikabidhiwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kalenga na Isimani, Caroline Utieno, katika hafla iliyoashiria mwanzo wa hekaheka za kinyang’anyiro hicho jimboni humoe.
Kiswaga aliwasili katika ofisi hizo akisindikizwa na Sekretarieti ya CCM ya Wilaya ya Iringa Vijijini, chini ya uongozi wa Katibu wa Wilaya, Sure Mwasanguti, tukio lililoonyesha mshikamano na nguvu ya chama chake kuelekea uchaguzi huo wa kidemokrasia.

