Kiswaga asaidia mifuko 200 ya Saruji Tosamaganga Sekondari

IRINGA: Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 100 ya shule ya sekondari Tosamaganga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga ilipo shule hiyo, Jackson Kiswaga, amekabidhi mifuko 200 ya saruji kwa shule hiyo kongwe kwa lengo la kuboresha mazingira ya elimu na michezo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Kiswaga amesema maadhimisho ya miaka 100 ya shule hiyo yanayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yatakuwa ya kihistoria na yatawakutanisha viongozi mbalimbali wa kitaifa, watu maarufu pamoja na wahitimu waliowahi kusoma Tosamaganga.

Baadhi ya viongozi wanaotarajiwa kushiriki ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, pamoja na viongozi wengine wa serikali, wadau wa elimu na alumni waliotokea katika shule hiyo yenye historia kubwa nchini.

Kiswaga amesema ataendelea kushirikiana na shule hiyo kutokana na kuwa sehemu ya ulezi wake kwa muda mrefu, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mazingira bora ya elimu ili kuwaandaa wanafunzi kuwa viongozi na wataalamu wa baadaye.

“Mbali na kusoma kwa bidii, wanafunzi wanapaswa kuwa watu wa vitendo, wenye nidhamu na wanaojituma. Mafanikio hayatokani na maarifa pekee, bali yanahitaji bidii, uthubutu na matumizi sahihi ya fursa zilizopo,” amesema Kiswaga.

Amesema mifuko hiyo ya saruji itasaidia maboresho ya uwanja wa mpira wa kikapu.

Katika hatua nyingine, Kiswaga amesema ameiagiza IRUWASA kuhakikisha huduma ya maji inapelekwa katika shule hiyo, huku akiahidi kufuatilia pia suala la upatikanaji wa taa ili kuboresha mazingira ya wanafunzi.

Aidha, ameipongeza serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo, ambapo zaidi ya Sh bilioni 1.6 tayari zimetolewa katika vipindi tofauti kwa ajili ya maboresho mbalimbali ya miundombinu.

Pia alimpongeza Diwani wa Kata ya Kalenga, Shakira Kiwanga, kwa mchango wake wa kuwaunganisha wadau wa maendeleo na kusaidia mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika shule hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Lauren Manga, amemshukuru Kiswaga kwa msaada huo akieleza kuwa utasaidia kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu na michezo kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Tosamaganga ni miongoni mwa shule kongwe nchini Tanzania, ikiwa imeanzishwa takribani miaka 100 iliyopita. Shule hiyo imekuwa kitovu cha kuzalisha wasomi, viongozi na wataalamu mbalimbali waliolitumikia taifa katika sekta tofauti.

Kwa miaka mingi, Tosamaganga imeendelea kujijengea heshima kutokana na taaluma, nidhamu na mchango wake katika maendeleo ya elimu nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button