Kiswaga atahadharisha mabadiliko tabianchi

DAR ES SALAAM: Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mhe. Jackson Kiswaga, ameeleza kuwa licha ya Serikali kuwekeza kiasi kikubwa cha takriban Sh trilioni 4 katika miradi ya maji, changamoto ya huduma hiyo bado ni kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko kubwa la watu.
Kiswaga aliyasema hayo wakati akitoa salamu zake kwenye Kongamano la Kitaifa kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE) katika Sekta ya Maji lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Akifafanua kuhusu hali halisi ya sekta hiyo, Kiswaga alikiri kuwa uwekezaji unaofanyika sasa ni mkubwa ukilinganisha na vipindi vilivyopita, lakini mahitaji yameongezeka mara dufu.
“Uwekezaji mkubwa kwenye maji umefanyika na sasa kuna miradi inayoendelea yenye thamani ya karibu Trilioni nne, Miradi zaidi ya 1,000 na kitu Lakini je, inakwenda kutatua changamoto za maji tulizonazo? Bado,” alieleza Kiswaga.
Alihitimisha kwa kuwatoa hofu wawekezaji akisisitiza kuwa Rais Dk, Samia Suluhu Hassan yuko tayari kuona sekta binafsi inashiriki kikamilifu kuleta maendeleo, na akalipongeza kongamano hilo kama fursa muhimu ya kuchangia mawazo ya jinsi ya kutatua changamoto za maji kwa pamoja kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.



