Kiswaga awafariji watoto yatima wa Tosamaganga

IRINGA: Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amewafariji watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Tosamaganga, kilichopo nje kidogo ya mji wa Iringa, kwa kuwapatia msaada wa mahitaji mbalimbali ya kibinadamu.
Katika ziara hiyo ya kugusa maisha ya wahitaji, Kiswaga alikabidhi msaada wa bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni za kufulia, mafuta ya kupikia, maji ya kunywa, vyakula vya aina mbalimbali, pampasi, pamoja na bidhaa nyingine muhimu za matumizi ya kila siku.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo, Kiswaga alisema:
“Mimi ni mbunge hadi Agosti 3, bunge litakapovunjwa rasmi kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Lakini siwezi kungoja mpaka muda huo kuhitimisha utumishi wangu bila kuwajali watoto hawa ambao ni kundi linalohitaji faraja, matumaini na msaada wa dhati kutoka kwa jamii.”
Aliongeza kuwa watoto hao licha ya kukosa walezi wa karibu, bado wana ndoto na haki ya kuishi maisha bora kama watoto wengine, hivyo ni wajibu wa kila mwanajamii kujitokeza kwa namna yoyote ile kusaidia makuzi yao.
“Watoto hawa si wa kituo hiki pekee, ni watoto wa jamii yetu. Na ninatoa wito kwa wadau, taasisi na watu binafsi kuendeleza moyo wa huruma kwa kuwasaidia watoto hawa na vituo vingine vya aina hii vilivyo katika mkoa wetu na nchi kwa ujumla,” alisema Kiswaga.
Kwa upande wake, Msimamizi wa kituo hicho, Sista Hellena Kiwele, alimshukuru Mbunge huyo kwa msaada huo muhimu na wa wakati, akisema kituo hicho kina jumla ya watoto 150, kati yao 85 wakiishi ndani ya kituo hicho cha malezi.
“Watoto wanaolelewa hapa ni kuanzia wenye umri wa chini ya mwezi mmoja hadi wale walioko kwenye hatua ya kwenda shule. Changamoto ni nyingi, hususan katika mahitaji ya kila siku ya chakula, usafi, afya na mahitaji ya kielimu,” alisema Sista Hellena.
Aliwaomba wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuwa kituo hicho kina mahitaji makubwa na ya kila wakati ambayo hakiwezi kuyakidhi peke yake bila msaada kutoka kwa jamii na mashirika mbalimbali.