Kitila abainisha uthabiti kiuchumi, kifedha

DODOMA – SERIKALI imesema katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu urari wa malipo yote ya nje uliimarika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema katika kipindi hicho, kulikuwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 1,616.4 ikilinganishwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 3,977.8 kwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Profesa Kitila alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa. Alisema mwenendo huo ulitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, kupungua kwa gharama za uagizaji bidhaa na huduma nje ya nchi.

“Kupungua kwa nakisi ya malipo ya nje ni ishara nzuri kwa uchumi wa nchi, kwani inaweza kuonesha kwamba nchi inakuwa na uwezo wa kudhibiti mahitaji yake ya fedha za kigeni na hata kujenga akiba ya fedha za kigeni. Hii ni muhimu katika kuhakikisha uthabiti wa kiuchumi na kifedha wa nchi,” alisema.

Profesa Kitila alisema urari wa biashara ya bidhaa kwa kipindi cha Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu ulikuwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 4,533 ikilinganishwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 5,597.9 kwa kipindi kama hicho cha mwaka 2023.

SOMA: Tril 15.94/- kugharimia shughuli za maendeleo

Aliwaeleza wabunge kuwa hali hiyo ilichangiwa na kupungua kwa bei ya mafuta ya petroli na kupungua kwa bei na kiasi cha bidhaa za mbolea.

“Bidhaa nyingi ziliagizwa kutoka China, India, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Japani na Afrika Kusini,” alisema.

Alisema hadi Machi mwaka huu thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi ilikuwa Dola za Marekani milioni 6,016.2, ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 5,629.2 kwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Ongezeko hili lilichangiwa zaidi na mauzo ya dhahabu na bidhaa asilia, hususani tumbaku, korosho na kahawa, pamoja na mauzo ya mazao ya mboga na maua. Aidha, bidhaa nyingi ziliuzwa India, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Uswisi na China.

Habari Zifananazo

Back to top button