Tril 15.94/- kugharimia shughuli za maendeleo

DODOMA – SERIKALI imetenga Sh trilioni 15.94 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema kati ya fedha hizo, Sh trilioni 12.30 ikijumuisha Sh trilioni 1.189 za ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya elimu ya msingi bure na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni fedha za ndani na Sh trilioni 3.640 ni za nje.

Profesa Kitila alisema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25.

Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 ni wa nne katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.

Profesa Kitila aliwaeleza wabunge kuwa uandaaji wa mpango huo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 na Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Miaka 15 wa mwaka 2011/12 – 2025/26.

Alisema serikali inaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambao ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Alisema serikali itaongeza ushirikiano na ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza na kugharimia miradi ya maendeleo kupitia njia bunifu na mbadala za ugharimiaji ikiwamo kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mpango wa Serikali 2024/25

Alisema lengo kuu la serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 ni kukamilisha programu na miradi ya maendeleo ya kielelezo na kimkakati iliyopo katika hatua za mwisho za utekelezaji hususani ambayo itawezesha sekta nyingine za kiuchumi na kijamii kustawi baada ya kukamilika.

Aliwaeleza wabunge kuwa utekelezaji wa mpango katika usimamizi wa uchumi jumla unalenga kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka asilimia ukuaji halisi wa asilimia 5.1 ya mwaka 2023.

SOMA: 2023: Idadi ya Watanzania yafika milioni 63.6

Profesa Kitila alisema shabaha nyingine ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika muda wa kati.

Malengo mengine ya mpango huo ni mapato ya ndani yafike asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 15.4 mwaka 2023/24.

Mpango unalenga kuongeza mapato ya kodi kufikia asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2024/2025 kutoka asilimia 12.6 ya mwaka 2023/2024.

Malengo mengine ni kuwa na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) isiyozidi asilimia tatu ya Pato la Taifa na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Vipaumbele Profesa Kitila alisema mpango utajielekeza katika maeneo matano ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa 2021/22-2025/26.

Maeneo hayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimaliwatu.

Profesa Kitila alisema msukumo zaidi umewekwa kukamilisha na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya miundombinu wezeshi katika sekta ya uchukuzi, usafiri na huduma za usafirishaji, sekta ya nishati, sekta ya mawasiliano na sekta ya maji.

Alitaja baadhi ya miradi ya kukamilisha ni mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), kukamilisha njia za kusafirisha umeme na vituo vya kupozea umeme, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima (Uganda) hadi Bandari ya Tanga eneo la Chongoleani na kuongeza kasi ya ujenzi na upanuzi wa mtandao wa mkongo wa mawasiliano wa taifa.

Habari Zifananazo

Back to top button