DODOMA – Idada ya watu nchini Tanzania ilikadiriwa kufikia 63,670,531 mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1 ukilinganisha na idadi ya watu milioni 61.74 waliotajwa katika matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema Tanzania Bara ilikuwa na watu milioni 61.7 sawa na asilimia 96.9 huku Tanzania Zanzibar ikiwa na watu milioni 1.9.
Akiwasilisha taarifa ya Hali ya Taifa ya Uchumi ya Mwaka 2023, Bungeni mjini Dodoma leo Juni 13, Waziri Mkumbo amesema wanawake bado wanaongoza wakikadiriwa kuwa 32,644,994, sawa na asilimia 51.3 ya watu wote na wanaume wakiwa 31,025,537.
“Makadirio ya mwaka 2023 ni maoteo ya mwenendo wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa kutumia mbinu ya kipeo,” amesema Prof. Mkumbo.
Mkoa wa Dar es Salaam umesalia kuwa na idadi kubwa ya watu wapatao milioni 5.6 ukifuatiwa na Mkoa wa Mwanza watu milioni 3.8.
SOMA: Deni la Taifa lafikia Sh trilioni 91.7
Serikali imesema idadi kubwa ya watu katika Mkoa wa Dar es Salaam imechangiwa na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na fursa za kiuchumi zinazovutia watu kuhamia kutoka mikoa mingine.
Mkoa wa Njombe ulikuwa na idadi ndogo ya watu wapatao 925,816. Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi ulikuwa na idadi kubwa ya watu wapatao 927,681, na huku Mkoa wa Kusini Unguja ulikuwa na idadi ndogo ya watu wapatao 203,646.
Msongamano wa watu Tanzania ulikuwa wastani wa watu 72 kwa kila kilometa ya mraba ikilinganishwa na wastani wa watu 70 mwaka 2022.
Waziri Mkumbo amesema msongamano wa watu Tanzania Bara ulikuwa wastani wa watu 70 kwa kila kilometa ya mraba ikilinganishwa na wastani wa watu 68 mwaka 2022. Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na msongamano mkubwa wa wastani wa watu 4,023 kwa kila kilometa ya mraba, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza uliokuwa na wastani wa watu 402 kwa kila kilometa ya mraba.
Vile vile, Mkoa wa Lindi ulikuwa na msongamano mdogo wa wastani wa watu 19 kwa kila kilometa ya mraba, ikifuatiwa na Mkoa wa Katavi uliokuwa na wastani wa watu 26 kwa kila kilometa ya mraba