TBS yatoa vyeti vya ubora viwanda 139

GEITA; SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeidhinisha, kuthibitisha na kutoa vyeti vya ubora kwa viwanda 139 vilivyopo mikoa ya kanda ya ziwa magharibi ambayo ni Geita, Shinyanga na Kagera.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Magharibi, Joseph Makene ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Geita na kueleza takwimu hizo kwa kipindi cha Septemba 2025 hadi Aprili 2026.
Makene amesema kati ya vyeti vilivyotolewa kuna vyeti vipya 41 huku vyeti 98 vikiwa ni vile ambavyo vimepitiwa, kukaguliwa na kuidhinishwa upya kwa wazalishaji wa bidhaa za viwandani.
“TBS inawahimiza wazalishaji wote wa bidhaa mbalimbali kuweza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na kuweza kupata leseni ya kutumia nembo ya ubora.
“Ukipata leseni ya kutumia nembo ya ubora, utakuwa umepanua soko lako, utaweza kusafirisha bidhaa zako Kwenda katika nchi ya Jirani na uhakika wa masoko ya ndani,” amesema Makene.
Makene ameeleza ukaguzi wa kina na elimu ya kutosha inaendelea kutolewa katika sekta ya vinywaji ambavyo vimechukua soko kubwa la watumiaji, ili kulinda ubora wa bidhaa sokoni.
“Wale wanaokiuka na tukathibitisha kwamba bidhaa zao hazina ubora, zile bidhaa tunaziteketeza kwa kuwa zikitumiwa na wananchi zinaweza kuwaletea madhara,” amesema Makene
Amewataka wakandarasi wa ndani na nje kuzingatia matumizi ya viwango elekezi vya Tanzania badala ya kutumia viwango vya nje katika miradi ya majengo na barabara.
“TBS ina maabara ambazo zinahusika na upimaji wa bidhaa za ujenzi zikiwemo mabati, nondo, na vitu mbalimbali vinavyotumika katika ujenzi,” amesema.
“Kwa hiyo tunawahimiza makandarasi kutumia maabara zetu ambazo zimehakikiwa, zimethibitishwa na zinapima bidhaa kulingana na kiwango cha kimataifa,” amesema Makene.



