Kituo cha afya Buzuruga chapatiwa vitanda
SERIKALI ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (KOICA) kwa kushirikiana na KOICA Alumni Tanzania (KOAT) imetoa msaada wa vitanda 10 vya hospitali vyenye thamani ya Sh milioni 9.5 kwa kituo cha afya cha Buzuruga Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Hatua hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania katika masuala ya afya.
Akizungumza katika hafla ya uchangiaji huo iliofanyika leo katika kituo hicho, Mkurugenzi wa Ofisi ya KOICA hapa nchini Manshik Shin amesema msaada huo umelenga kusaidia utoaji wa huduma za afya kila siku katika kituo cha afya cha Buzuruga.
“KOICA, kupitia KOICA Alumni Tanzania (KOAT), inapenda kuwapongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya.” Amesema Shin.
Kwa upande wake, Rais wa KOAT, Dk Deman Yousuf, amesema Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia KOICA na KOICA Alumni Tanzania (KOAT) wamekuwa wakishirikiana na Serikali ya Tanzania.
Naye mganga mfawidhi wa kituo cha afya ya Buzuruga William Ntinginya ameshukuru kwa msaada huo wa vitanda.
Amesema kwa sasa kituo chao cha afya kina uhitaji wa vitanda 42 kwajili ya kutatua tatizo la vitanda kwa wodi ya mama na mtoto.
Ameiomba KOICA iwasaidie katika upatikanaji wa mashine kubwa ya kufulia kwajili ya kuweza kufua mashuka ya mama na mtoto.
‘’KOICA tunaomba itusaidie katika ujenzi jengo la kutolea damu ili liweze kuwasaidia mama wajawazito. Kwa mwezi katika kituo chetu cha Afya tunapokea wanawake wajawazito 600 kwajili ya kujifungua’’ amesema Ntinginya.