Kituo cha taarifa chaokoa ndoa zilizoyumba Kalenga

Kituo cha Taarifa na Maarifa ya Masuala ya Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kinachofanya kazi kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kimefanikiwa kushughulikia na kusuluhisha migogoro mikubwa ya ndoa nane katika Kata ya Kalenga, wilayani Iringa.

Mwenyekiti wa kituo hicho Rose Wikiso amesema migogoro hiyo, ambayo awali ilishindikana kutatuliwa kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii na hata kukwama katika vyombo vya sheria, hatimaye wameitatua kwa kipindi kifupi.

Hatua hiyo amesema imesaidia wenza kurejesha upendo na kuimarisha uhusiano wao ndani ya familia.

“Tuliona sababu nyingi za migogoro hiyo zinatokana na masuala ya kiuchumi, ambapo wanandoa wanashindwa kugawana majukumu ipasavyo, na hii inapelekea migogoro mikubwa katika ndoa,” amesema.

Amegusia pia, mahusiano nje ya ndoa akisema yamekuwa chanzo kikubwa cha ndoa nyingi kuingia katika migogoro na hata kuvunjika, hali inayosababisha maumivu kwa familia.

Amesema, kazi ya kutoa ushauri inayofanywa na kituo chao, mafunzo ya haki za kijinsia, na usuluhishi wa migogoro kwa wanandoa, inachangia kubadili mtazamo wa wanajamii kuhusu ndoa na majukumu ya kila mmoja.

“Kupitia majadiliano na wanandoa, tumefanikisha maridhiano katika ndoa hizi nane na kuzuia kuzorota kwa maisha ya familia na watoto wao,” alisisitiza.

Mbali na changamoto za ndoa, amesema kituo kimebaini ongezeko la kina mama wanaozaa lakini hawataki kuolewa, jambo ambalo limeleta mjadala mkubwa kuhusu ukatili wa kijinsia na malezi ya watoto katika familia za mzazi mmoja.

Mmoja wa viongozi wa dini katika kata hiyo, Zuberi Witala anaeleza kuwa baadhi ya wanawake wanaamua kutopendelea ndoa kutokana na hofu ya ukatili wa kijinsia, ukosefu wa uhuru wa kiuchumi, au uzoefu mbaya wa ndoa za awali.

“Hili ni tatizo linaloathiri watoto zaidi, kwani malezi ya mzazi mmoja mara nyingi yanakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo uhaba wa rasilimali na ukosefu wa msaada wa kimalezi kutoka kwa baba wa mtoto,” amesema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa tatizo hili linapaswa kushughulikiwa kwa njia jumuishi kwa kuhakikisha elimu ya haki za kijinsia inatolewa kwa vijana ili kujenga uelewa wa umuhimu wa usawa katika mahusiano na familia.

Pia, anahimiza jamii kuhakikisha kuwa wanaume wanawajibika kwa watoto wao hata kama hawajaamua kuoa.

“Ukatili wa kijinsia haupo tu katika hali ya kawaida tunayoijua kama vipigo, bali pia katika mfumo wa kiuchumi na kihisia. Tunapaswa kuelimisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia na kusaidia wanawake kujitegemea kiuchumi ili kuepusha utegemezi ambao mara nyingi huleta migogoro,” amesema.

Baadhi ya wanaharakati wameeleza kuwa migogoro ya ndoa na ongezeko la kina mama wanaozaa bila kutaka kuolewa vinahusiana kwa karibu na hali ya kiuchumi na kijamii.

Mwenyekiti wa mashirika yasio ya kiserikali mkoani Iringa (Iciso), Raphael Mtitu amesema ukosefu wa ajira, utegemezi wa kifedha, na ukosefu wa elimu ya jinsia vinafanya wanawake kushindwa kujiimarisha, hivyo kuwa katika mazingira yanayowafanya waathiriwe na ukatili wa kijinsia.

Mtitu amesema wanawake wengi katika ndoa hukumbana na ukatili wa kihisia na kiuchumi, ikiwemo kunyimwa rasilimali, kutengwa kihisia, au kunyimwa tendo la ndoa kama njia ya kuwafanya waishi kwa hofu au utegemezi.

Hali hiyo amesema inasababisha ndoa nyingi kuwa na migogoro, na wanawake wengine kuamua kutokuwa katika ndoa kabisa ili kujilinda.

Naye mwanahabari Francis Godwin amesema ongezeko la wanawake wanaozaa nje ya ndoa linapaswa pia kuangaliwa kutoka kwa upande wa wanaume.

“Baadhi ya wanaume hujihusisha kimapenzi lakini wapenzi wao wanaposhika mimba, hukwepa majukumu. Kwa hivyo, suala hili si la wanawake pekee bali linahitaji mabadiliko ya mitazamo kuhusu majukumu ya uzazi kwa pande zote mbili,” amesema.

Godwin amependekeza elimu kuhusu usawa wa kijinsia ipewe kipaumbele, hasa kwa vijana ili kupunguza dhana potofu kuhusu ndoa, mahusiano, na majukumu ya kifamilia.

“Pia, programu za kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi zinaweza kusaidia kupunguza utegemezi na hivyo kupunguza migogoro ya ndoa inayotokana na masuala ya kifedha,” amesema.

Kwa mtazamo wa wanaharakati hao, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa sheria za ulinzi wa haki za wanawake na watoto zinatekelezwa ipasavyo. Hii inahusisha kuhakikisha kuwa wanaume wanaowatelekeza watoto wanachukuliwa hatua, na pia kuongeza nguvu ya msaada wa kisheria kwa wanawake wanaoathiriwa na ukatili wa kijinsia ndani ya ndoa.

Kwa ujumla, wanaharakati hao wamesisitiza kuwa kutokomeza ukatili wa kijinsia ni jukumu la jamii nzima.

“Elimu, sera madhubuti, na ushirikiano kati ya wadau mbalimbali vinaweza kusaidia kupunguza changamoto hizi kwa manufaa ya wanawake, wanaume, na watoto,” amesema Mtitu.

Mmoja wa maafisa maendeleo ya jamii mkoani Iringa ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kushughulikia changamoto hizo.

Hatua hizo ni panoja na kuimarisha sera na Sheria za kulinda haki za wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kwa kuzingatia changamoto mpya za kijamii, ikiwa ni pamoja na ndoa zinazovunjika kwa sababu za kiuchumi na usaliti.

Hatua nyingine ni kuanzisha na Kuboreshwa kwa mifumo ya msaada wa kisaikolojia na kisheria kwa wanawake na wanaume walioko kwenye ndoa zenye migogoro, ili kuwapa nafasi ya kupata ushauri bila kuogopa unyanyapaa wa jamii.

Na kwa kupitia idara ya ustawi wa jamii, afisa huyo amesema serikali inashirikiana na mashirika ya kiraia kuimarisha upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa wanawake wanaohitaji msaada wa talaka, matunzo ya watoto, au haki zao ndani ya ndoa.

Amesema kuanzisha au kuimarisha programu za kuwawezesha wanawake kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mikopo yenye riba nafuu, mafunzo ya ujasiriamali, na fursa za ajira inasaidia kupunguza utegemezi wa wanawake kwa waume zao.

Afisa huyo amezungumzia pia programu maalum za elimu katika shule na vyuo kuhusu haki za kijinsia, ndoa, na wajibu wa wanandoa katika jamii, na kampeni ya vyombo vya habari, inayohamasisha umuhimu wa ndoa zenye usawa, wajibu wa wazazi, na athari za ukatili wa kijinsia.

Kuhusu kushirikiana na wadau wa kijamii kupunguza unyanyapaa dhidi ya kina mama wasiotaka kuolewa, wanaharakati wametoa ushauri kwa serikali kushirikiana na taasisi za kijamii na dini kuhamasisha jamii kuhusu changamoto za familia za mzazi mmoja na umuhimu wa kusaidia watoto kupata malezi bora.

“Hii iende sambamba na kuweka mifumo bora ya ufuatiliaji kuhakikisha kwamba watoto wanaozaliwa nje ya ndoa wanapata haki zao, ikiwa ni pamoja na huduma bora za afya, elimu, na matunzo ya kifamilia, ” amesema mwanasheria Baraka Kimata.

Kwa kuchukua hatua hizi Kimata amesema migogoro ya ndoa itapungua, ustawi wa wanawake na watoto utaimarika, na hivyo kusaidia kupunguza ukatili wa kijinsia katika jamii.

Kituo cha Taarifa na Maarifa kinaendelea kushirikiana na TGNP na wadau wengine wa haki za kijinsia ili kutoa ushauri, na mafunzo kwa jamii, kwa lengo la kuondoa ukatili wa kijinsia na kuhakikisha familia zinakuwa na mahusiano imara kwa ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, wanachama wa kituo hicho wamesema kuwa ukosefu wa rasilimali fedha umekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hali inayopunguza ufanisi wa shughuli zao.

Kutokana na changamoto hiyo, wameomba wadau mbalimbali kujitokeza na kutoa msaada ili kuwawezesha kuimarisha utendaji wao na kufanikisha malengo yao kwa ufanisi zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button