Majaliwa azindua kiwanda cha kuchakata maziwa Katavi

Majaliwa azindua kiwanda cha kuchakata maziwa Katavi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua kiwanda cha kuchakata maziwa cha MSS kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkoani Katavi ambacho kina uwezo wa kusindika wastani wa lita 10,000 kwa saa.

Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake umegharimu shilingi milioni 600, Majaliwa amesema kuwa Rais  Dk Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, ili kila mwenye uwezo awekeze.

Amesema hayo leo Desemba 13, 2022, wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinazalisha maziwa ya mtindi na maziwa freshi na kinatarajia kuanza uzalishaji wa samli hivi karibuni.

Advertisement

Pia ametoa rai kwa wafugaji wanaozunguka kiwanda hicho kuuza maziwa kwa mwekezaji huyo, ili waweze kujiongezea kipato na kumwezesha mwekezaji huyo kuwa na uhakika wa malighafi ya kutosha.

“Huyu Bwana Maliki anamuunga mkono Rais Mheshimiwa Dkt. Samia katika nia yake ya kuendeleza uwekezaji nchini. Uwepo wa kiwanda hiki kunaisaidia kuendeleza  mkakati wa lishe bora kwa kila Mtanzania, kwa sasa tunamshauri aendelee kupanua kiwanda hiki, ili aongeze uzalishaji na wananchi wengi wazidi kupata ajira.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kuwa Rais Dk. Samia ameridhia kutoa shilingi milioni 200 kupitia Bodi ya Maziwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukusanyaji wa maziwa Mpanda, Katavi.

“Vituo hivi vitajengwa takribani kumi nchi nzima na kila kimoja kitagharimu shilingi milioni 200.”

Ameongeza kuwa Rais Dk Samia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitamba ya maziwa 500 na madume ya nyama 500 ambayo yatagawiwa nchi nzima, lengo likiwa ni kuboresha aina ya mifugo inayofugwa na wananchi.

1 comments

Comments are closed.