Klabu za haki za binadamu zaasisiwa shuleni Iringa

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imefanya ziara katika shule 11 za sekondari mkoani Iringa na kutoa elimu juu ya haki za watoto na kuhamasisha wanafunzi kuunda klabu za haki za binadamu.
Katika ziara hiyo, wanafunzi wamefundishwa kuhusu haki zao, wajibu wao, na namna ya kujilinda dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa aina yoyote.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kidamali, Mwalimu Yoram Mponzi, ambaye shule yake ina zaidi ya wanafunzi 850, amesema mpango huo umekuwa wa manufaa kwa wanafunzi kwani utawasaidia kujitambua na kuelewa thamani yao katika jamii.
Kamishna wa Haki za Binadamu, Thomas Masanja, amesema kuwa klabu za haki za binadamu zitakuwa chini ya uangalizi wa walimu wawili—mmoja wa kike na mwingine wa kiume—na uanachama wake utakuwa wa hiari.
Alisema lengo ni kuhakikisha watoto wanapata elimu ya kutosha kuhusu haki zao na namna ya kuzitetea.
“Tunataka ushiriki wa watoto katika kujifunza haki za binadamu na utawala bora. Ninyi ni viongozi wa kesho, hivyo ni lazima mjifunze haki zenu mapema ili kuweza kuzitetea katika jamii,” alisema Kamishna Masanja.
Ofisa wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Frolence Chaki, aliwaeleza wanafunzi kuwa haki za mtoto zimegawanyika katika makundi makuu manne ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi – mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha maisha yake.
Nyingine ni haki ya kuendelezwa – mtoto anatakiwa kupata elimu, huduma za afya, lishe bora, na malezi mazuri, haki ya kulindwa – mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya ukatili, unyanyasaji wa kijinsia, kazi hatarishi, ndoa za utotoni, na unyonyaji wa aina yoyote.

Alisema kundi la nne linahusu Haki ya kushiriki – mtoto ana haki ya kushiriki maamuzi yanayomhusu kwa mujibu wa umri na uwezo wake.
“Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vyote vya ukatili. Ikiwa ni unyanyasaji wa kijinsia, kazi za hatari, au ukatili wa aina yoyote, ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha usalama wao,” amesisitiza Chako.
Aliwataka wanafunzi kuepuka vitendo viovu na kuwa na nidhamu shuleni. Pia, aliwaasa kutojihusisha na matumizi mabaya ya simu za mkononi, akibainisha kuwa matumizi mabaya ya teknolojia yanaweza kuathiri mustakabali wao.
Katika mikutano hiyo, baadhi ya wanafunzi walieleza hofu yao kuhusu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyofanywa na baadhi ya ndugu, walimu, na watu wa karibu.
Kamishna Masanja alieleza kuwa vitendo vya ulawiti, ubakaji, na unyanyasaji wa kijinsia havipaswi kufumbiwa macho, na jamii inapaswa kushirikiana kuripoti wahusika kwa vyombo vya sheria.
“Tukifumbia macho vitendo vya ukatili, hatutakuwa na kizazi chenye maadili huko mbele. Wazazi na walimu wanapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya manyanyaso ya kijinsia,” alisema Masanja.
Kuhusu ajira kwa watoto, Tume ilifafanua kuwa mtoto anaweza kushiriki kazi ndogo ndogo zinazomfundisha kujitegemea, lakini ajira za watoto zinazomhatarisha kimwili, kiakili, au kisaikolojia ni marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa (ILO) na za ndani ya nchi.
Katika mjadala na makundi ya kijamii, baadhi ya wazazi wamelalamikiwa kuchangia uharibifu wa watoto wao kwa kuwakingia kifua wanapofanya makosa.



