Klabu zisaidie kuzalisha wachezaji bora Taifa Stars

MICHUANO ya Mabingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) kwa upande wa Tanzania ilimalizika Ijumaa baada ya Taifa Stars kufungwa bao1-0 na Morocco, hivyo kutolewa kwenye hatua ya robo fainali Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hii ni rekodi kwa Stars kwani katika historia yake si tu kwenye michuano ya CHAN, bali hata ile ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) haijawahi kufika hatua hiyo.

Stars imeshiriki mara tatu fainali za Afcon; mwaka 1980 Lagos, Nigeria, 2019 Cairo, Misri na 2023 Abidjan, Ivory Coast lakini awamu zote hizo iliishia hatua ya makundi.

SOMA: Tanzania yataka uenyeji Afcon 2026/27

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadau wake yaani klabu zote za Tanzania wanapaswa kujifunza kutokana na ushiriki huo kwenye fainali hizi ambazo Tanzania imekuwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda.

Kutokana na ushiriki huo kwenye ardhi ya nyumbani; wadau wajiulize wapi nchi imekwama, sababu gani zilisababisha Taifa Stars ikaishia njiani na nini kifanyike ili ifanikiwe zaidi kwenye michuano ijayo.

Yote haya yapo ndani ya uwezo wa TFF na wadau wake wote hususani klabu za soka Tanzania ambazo ndizo huzalisha wachezaji wa timu ya taifa.

TFF ni msimamizi mkuu wa Taifa Stars lakini isivyo bahati, haimiliki wachezaji bali hutengeneza mazingira mazuri kuhakikisha mpira wa miguu unachezwa.

Tunachotaka kusema ni kwamba klabu zinabeba dhima kubwa ya kuhakikisha zinazalisha wachezaji wenye viwango bora, ambao watateuliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mashindano yajayo na zaidi michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) itayoanza Desemba mwaka huu nchini Morocco na tutakapokuwa wenyeji mwaka 2027.

Klabu zinapaswa kuzalisha wachezaji wenye vipaji bora zaidi ambao watachaguliwa kuitumikia Stars kwenye mashindano mbalimbali hasa yaliyo mbele yetu ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026, Afcon itakayoanza Morocco Desemba mwaka huu na Afcon 2027.

Klabu zitengeneze mifumo mizuri ya kung’amua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi ambao watazisaidia klabu zao kwenye mashindano mbalimbali ambapo wengine wanaweza kuuzwa nje ya nchi na faida itakuwa kuchaguliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Ukiangalia kikosi cha sasa kwa umakini utagundua bado kwa kiwango kikubwa kinategemea nyota walewale ambao walivumbuliwa zaidi ya miaka mitano hadi 10 nyuma, hauoni kama kuna nyota wengi wanaoweza kuja kuchukua nafasi au kutoa ushindani kwa wazoefu hao kwenye kikosi cha timu hiyo.

Unawazungumzia wachezaji kama kipa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, Feisal Salum, Mudathir Yahya na Hamadi Hilika ambao miaka nenda rudi wamekuwa wakiendelea kuwa muhimili wa timu hiyo.

Tunatamani kuona vipaji vingi zaidi vinaibuliwa na klabu kwa faida ya timu ya taifa kwenye mashindano mbalimbali. Bado hatujachelewa na hivi karibuni Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Septemba 17, mwaka huu tunaamini klabu zitawapa nafasi zaidi wachezaji chipukizi kwa lengo la kuwaimarisha ili waje kuwa na mchango kwenye kikosi cha Stars.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button