Kongamano la ne MUCE: AI, tafiti na ufundi stadi mjadala mkubwa

CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimefanya kongamano lake la nne la kimataifa likiwaleta pamoja wataalamu, watafiti, wanataaluma na wadau kutoka ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Method Samwel amesema lengo la kongamano hilo lililofanyika kwa siku mbili lilikuwa ni kuwasilisha tafiti bunifu, kubadilishana uzoefu na kujadili masuala muhimu ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii.

Profesa Samwel amesema tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu hazipaswi kubaki katika karatasi bali zinapaswa kuwasilishwa kwa jamii ili zitumike kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi.

“Tunafanya tafiti nyingi zinazolenga kuongeza thamani ya mazao, kuboresha huduma za kijamii na kutatua changamoto za maendeleo. Sasa tunaanza kuzitekeleza wenyewe kivitendo kama sehemu ya mafunzo na ufanisi wa tafiti hizo,” amesema Profesa Samwel.

Ameongeza kuwa tafiti hizo si tu zinasaidia jamii kuboresha kipato na maisha, bali pia zinachangia pato la taifa na kwamba chuo kimeanza kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha matokeo ya tafiti hayaishii darasani bali yanaingia kwenye utekelezaji wa sera, biashara na huduma za kijamii.

Akizungumzia matumizi ya teknolojia mpya kama Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI), Profesa Samwel amesema ingawa awali kulikuwepo na hofu kuwa AI ingeathiri uwezo wa wanafunzi kufikiri au hata kuchochea wizi wa kazi za kitaaluma, MUCE imechukua hatua madhubuti kulinda ubora wa elimu.

“Tuna muongozo wa kuzuia wizi wa kitaaluma na tumeanzisha mafunzo kwa wahadhiri na wanafunzi kuhusu matumizi bora ya AI katika ufundishaji na ujifunzaji,” amesema.

Aidha, amesema Serikali kupitia ufadhili wake imetoa zaidi ya dola za Kimarekani milioni nane kuboresha miundombinu ya teknolojia chuoni hapo, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuongeza ubora wa ufundishaji.

Katika kongamano hilo, suala la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu liligusiwa kwa kina, ambapo Profesa Samwel amesema MUCE inaendelea kuboresha programu zake ili kuwawezesha wanafunzi kujiajiri kupitia maarifa na ujuzi wa vitendo.

“Tunaondoa dhana potofu kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu hawezi kwenda VETA – bali, anaenda kuongeza thamani ya digrii yake,” amesema.

Aidha, Profesa Samwel ameeleza kuwa ni vyema walimu wahitimu wakafanyiwa usaili hasa panapokuwa na nafasi chache kama ilivyo kwa wanataaluma wa kada nyingine ili kuwapata katika ajira mpya wale walio bora zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa MUCE, Dk Selina Mkimbili amesema kongamano hilo linaangazia njia za kuhakikisha tafiti na bunifu zinazofanyika chuoni hapo zinavuka mipaka ya chuo na kuingia sokoni, viwandani na mashambani.

Katika kuonesha mwelekeo mpya wa elimu ya juu, amesema ni muhimu elimu iwe ile yenye msingi wa utafiti, ubunifu, teknolojia na ujuzi wa vitendo.

“Tuna wadau kutoka nje na ndani ya nchi, tunawahitaji washirikiane nasi ili tafiti zetu zitafsiriwe katika bidhaa, huduma na suluhisho la changamoto za jamii,” amesema Dk Mkimbili.

Naye Dk Japhace Poncian mratibu wa kongamano hilo, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza tafiti na ubunifu kuelekea kwenye biashara, akisema vyuo vikuu vinapaswa kuwa madaraja ya maendeleo, siyo magereza ya maarifa.

“Bila ushirikiano wa vyuo na wadau, tutabaki na taarifa zisizofika popote. Tunahitaji mazingira rafiki ya kushirikiana na sekta binafsi, viwanda na jamii kwa ujumla,” amesema.

Sarah Mwaipopo, mwanafunzi wa mwaka wa tatu na Waziri Mkuu Mstaafu wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, amesema elimu inayotolewa chuoni hapo pamoja na kongamano hilo ni nyenzo muhimu kwao kutambua fursa na kuzitumia kwa maendeleo ya kibinafsi na jamii.

“Kupitia elimu na tafiti, nikirudi kwenye jamii naweza kuwasaidia wengine, huku nikitambua fursa zilizopo na namna ya kuzitumia vizuri,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button