Kongamano laibua hoja ufanisi wa huduma za maji

DAR ES SALAAM: Kongamano la Kitaifa kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika Sekta ya Maji lililofanyika Mei 9, 2026 jijini Dar es Salaam limeibua mjadala kuhusu changamoto za ufanisi, ucheleweshaji wa huduma na mianya ya rushwa katika mamlaka za maji nchini ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Akiwasilisha mada, Lettice Rutashobya, aliyewahii kuhudumu Bodi ya Dawasco kwa miaka sita, alisema bado kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa huduma za maji licha ya uwepo wa taasisi na wataalamu wa kutosha.
Kwa upande wake, Profesa Rutashobya alisikitishwa na kasi ndogo ya kushughulikia hitilafu za miundombinu, hususan mabomba yanayovuja na kuchelewa kwa huduma za matengenezo, hali inayochangia upotevu mkubwa wa maji na usumbufu kwa wananchi.
“Kama wahandisi hawatoshi, na inachukua mwaka mmoja au hata miwili kurekebisha bomba linalovuja, basi kuna haja ya kujiuliza kwa nini tusitumie mfumo tofauti na kuipa nafasi sekta binafsi kusaidia,” alisema Profesa Rutashobya.
Mbali na changamoto za kiufundi, Profesa huyo pia alifichua kuwepo kwa vitendo vya ukosefu wa uadilifu vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa chini, ambapo wananchi hudaiwa fedha zisizo rasmi kwa madai ya kununua vifaa vya kuunganishiwa huduma za maji.
Profesa Rutashobya aliiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa mfumo wa PPP katika sekta ya maji ili kuvutia uwekezaji, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wake, ushiriki wa sekta binafsi unaweza kusaidia kuongeza kasi ya matengenezo ya miundombinu, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji nchini.



